Na John Walter -Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ametangaza marufuku kwa walimu wakuu kupanga viwango vya fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni bila kushirikisha wazazi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mtaa wa Komoto Mjini Babati, Sendiga ameeleza kuwa utaratibu huo unapaswa kufanyika kwa uwazi na kushirikisha kamati za wazazi katika shule husika.
Sendiga amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kuandaa vikao na kamati za wazazi, ambavyo vitahusisha maafisa lishe wa halmashauri, ili kutoa elimu juu ya umuhimu wa chakula kwa maendeleo ya watoto shuleni.
"Kwenye vikao hivyo wahudhurie maafisa lishe wa halmashauri ili watoe elimu kwa wazazi, nini umuhimu wa watoto wao kupata lishe shuleni?" alisema Sendiga.
Amesisitiza kwamba ushirikiano wa pande zote ni muhimu kwa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kwa ajili ya maendeleo yao ya kielimu.
Aidha hatua hiyo ya mkuu wa mkoa inalenga kuboresha uwajibikaji na kuhakikisha wazazi wanashiriki kikamilifu katika kuboresha lishe ya watoto shuleni.
0 Comments