Na John Walter -Babati
Mtoto wa kike Neema Paskali (3) mkazi wa Kijiji cha Lalaji Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, amejeruhiwa vibaya maeneo ya uso na kichwa baada ya kushambuliwa na mnyama Fisi akijikinga na mvua nyumbani kwao.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jioni ya Desemba 14,2024 ambapo fisi huyo alimjeruhi mtoto huyo akiwa kwenye zizi la mifugo alipokimbilia kujisitiri asiloane na mvua iliyokuwa inanyesha wakati huo huku wazazi wakiwa ndani.
Kwa mujibu wa baba mdogo wa mtoto huyo, Paulo Walaa, fisi huyo aliingia ghafla kwenye banda hilo alipokuwa Neema na kumfanyia shambulizi hilo lililosababisha mtoto huyo kukosa jicho lake moja.
Ameeleza kuwa pia Baba yake Neema amejeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake wakati akimdhibiti Fisi huyo, huku mama mzazi akipoteza fahamu.
Mtoto Neema alikimbizwa haraka katika zahanati ya Kijiji cha Lalaji na kupewa rufaa ya kwenda hospitali ya wilaya ya Hanang' Tumaini kisha baadaye katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, ambako anaendelea kupatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa hospitali ya Rufaa mkoa wa Manyara ambaye amemhudumia Neema, Dr. Leandry Malisa, ameeleza kuwa hali yake bado ni mbaya na wamempa Rufaa ya kwenda kutibiwa katika hospitali ya Benjamin William Mkapa Mkoani Dodoma walipo Madaktari wengi bobezi na kwamba matibabu yake yatachukua muda mrefu.
Neema kwa sasa anapua kwa kutumia mashine kwani mfumo wake wa hewa umeharibika.
Wazazi wa Neema hawana uwezo wa kifedha hivyo wanakuomba wewe uliye na mapenzi mema na moyo wa huruma na upendo uwasaidie kwa kiasi chochote utakachojaliwa ili mwanao apone na arejee katika hali yake ya kawaida.
Mawasiliano ya Baba mdogo wa Neema Paulo Wallah, ni 0718044142.
0 Comments