Na John Walter -Babati
Wanawake Polisi Mkoa wa Manyara wameungana na dunia kuadhimisha kilele cha Siku 16 za Kupinga Ukatili kwa njia ya vitendo vya huruma na kuhamasisha jamii kupinga vitendo hivyo.
Katika maadhimisho haya, walitoa misaada kwa kituo cha kulea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kiitwacho Hossana kilichopo Managhat wilayani Babati, wakionesha mfano wa upendo na mshikamano kwa jamii.
Misaada hiyo ilihusisha chakula kama vile mahindi, maharage,mchele, mafuta ya kupikia na ya kujipaka, vinywaji pamoja na sabuni za kufulia, vyote vikilenga kuboresha watoto hao.
Wanawake hao walionyesha kuwa jukumu la kupambana na ukatili linaweza kuanza kwa matendo madogo yanayojenga matumaini kwa wale walioathirika zaidi.
Mbali na kutoa misaada, walifanya kampeni ya kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto, na aina nyingine za ukandamizaji. Walisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kuimarisha ulinzi na usalama wa makundi yaliyo hatarini.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Kamishna msaidizi wa polisi Lucas Mwakatundu amesema wanapoadhimisha siku 16 wanatuma ujumbe wa matumaini kwa wahanga wa ukatili na kuiasa jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha Manyara panakuwa salama bila matendo hayo.
Aidha Mwakatundu ametoa wito kwa viongozi wa kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika juhudi za kumaliza ukatili, huku wakihamasishwa kuripoti matukio ya ukatili na kusaidia wahanga kupata msaada unaostahili.
Akikabidhi misaada hiyo mkuu wa Polisi wilaya ya Babati na Mwenyekiti wa mtandao wa Polisi Wanawake wilayani humo SP Ernesta Mwambinga, amewasihi wananchi wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia shughuli za ujenzi zinazoendelea na misaada mingine.
Maadhimisho haya ni sehemu ya juhudi za Wanawake Polisi Manyara kuhakikisha mabadiliko chanya katika jamii yanapatikana kupitia mshikamano, huruma, na vitendo vya kujenga.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto polisi mkoa wa Manyara Afande Wilnes Kimario naye aliongozana na jopo hilo kutoa Misaada hiyo.
Kaulimbiu ya Mwaka huu, Kuelekea miaka 30 ya Beijing, chagua kutokomeza Ukatili wa kijinsia.
0 Comments