F Rais Dkt Samia aongoza shughuli ya kuuaga mwili wa Dr Ndugulile. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Rais Dkt Samia aongoza shughuli ya kuuaga mwili wa Dr Ndugulile.


Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameongoza shughuli ya kuuga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Dkt. Fautine Ndugulile katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Akitoa salamu za pole, Mheshimiwa Rais alisema licha ya kifo cha Dkt. Ndulile lakini ameweka heshima kwa Tanzania kutokana na nafasi aliyoipata katika Shirika la Afya Duniani.

Amesema kuondoka kwake ni kugumu lakini hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu na kutaka Watanzania kulipokea jambo hilo.

“Sisi wanadamu tunapanga lakini Mungu naye anapanga yake, kazi ya Mungu haina makosa, tumshukuru kwa uhai  na zawadi ya maisha yake, tutaendelea kumuombea na kuiweka familia yake kwenye maombi.

“Marehemu Dkt. Ndugulile ameweka heshima katika nchi yetu kwa kupata nafasi WHO, niseme kwamba Mungu amechukua amana yake lakini kwetu sisi ni kuendelea mbele tena kwenye ushindani wa nafasi hiyo”. alisema.

Mheshimiwa Rais alisema Tanzania itatafuta mgombea mwingine mwenye sifa zinazoweza kushindana na ulimwengu  na kuingia tena kwenye ushindani kwa nguvu ile ile ili kuweka heshima ya nchi.

Alisema ni wajibu wa nchi kuhakikisha Watanzania wabobezi wanawekewa nguvu ili waweze kuwakilisha katika fani za kimataifa kama walivyofanya kwa Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.

“Mheshimiwa Dkt. Ndugulile aligombea, Serikali ikamuunga mkono na akapata,hata hivyo Mwenyezi Mungu hakutaka iwe hivyo na leo tunamuaga mwenzetu na hatujui sisi safari yetu ni lini maana tunakuja na kuondoka”, alisema. 

Mheshimiwa Samia alitoa pole kwa familia ya marehemu akiwemo mama mzazi, mke na Watoto, wananchi wa Kigamboni, Bunge, Chama cha Madaktari Tanzania na Watanzania kwa ujumla.

Aidha, alitoa shukrani kwa salamu za pole ambazo amepokea kutoka kutoka mashirika ya Kimataifa, Afrika na Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika.

Mheshimiwa Dkt. Ndugulile alifariki tarehe 27 Novemba, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Post a Comment

0 Comments