F Serikali yazindua kituo jumuishi kuwahudumia walioathiriwa na ukatili. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yazindua kituo jumuishi kuwahudumia walioathiriwa na ukatili.



Na John Walter-Manyara

Katika kuhakikisha jamii inabaki salama dhidi ya Ukatili, Serikali mkoani Manyara imezindua kituo jumuishi cha mkono kwa mkono (one stop center) katika hospitali ya Rufaa ya mkoa kitakachotumika kutoa huduma za kitabibu na ushauri nasaha kwa watoto waliofanyiwa ukatili.

Kituo hicho, ambacho ni cha kwanza katika mkoa huo, kinalenga kutoa huduma za kisaikolojia, msaada wa kisheria, na huduma za afya kwa watoto waliokumbwa na ukatili wa aina mbalimbali, ikiwemo ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kimwili, na kihisia.

Akizungumza katika hafla hiyo desemba 6,2024 , mgeni rasmi wa shughuli hiyo Mkurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu Merkion Ndofi ambaye amemwakilisha Katibu mkuu wa wizara Maendeleo ya Jamii jinsia Wanawake na makundi maalum, ameupongeza uongozi wa mkoa pamoja na wafanyakazi wa shirika la Elizabeth Glacer Paediatric Foundation- EGPAF kwa jitihada wanazofanya za kupinga Ukatili kwenye jamii.

"Kipekee napenda kuwapongeza Sana kwa hatua mliyochukua ya kusaidia jamii kupambana na kuzuia ukatili dhidi ya watoto, kimsingi ukatili dhidi ya watoto unapelekea mtoto kuathirika kisaikolojia, kupata madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu" alisema Ndofi 

Amesema kuwa serikali inaendelea kushughulikia mashauri dhidi ya Wanawake na watoto ikiwemo ukatili wa Kimwili, kihisia, kingono na kiuchumi kipindi cha Julai 2022 Hadi Juni 2024 ambapo kupitia jeshi la polisi imeboresha utendaji wa madawati ya polisi ya jinsia na watoto 460 yaliyopo katika vituo mbalimbali vya polisi nchini na hadi sasa yamepokea na kushughulikia jumla ya mashauri 30,045 ya Ukatili.

Akisoma taarifa ya Maendeleo ya hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dr Yesige Mutajwaa amesema changamoto zinazosababisha vitendo vya ukatili viongezeke ni pale ambapo kesi nyingi za ukatili zinarudishwa nyumbani na ndugu wanamalizana wao kwa wao lakini kama hospitali licha ya changamoto hizo wameendelea kufanya jitihada kubwa za kuboresha huduma kwa waathiriwa wa ukatili ili kulinda ushahidi.

"Changamoto kubwa ni kesi kurudishwa nyumbani kwa kutumia faini na sheria za kimila, kwa sasa tunawezesha vituo vingine vinavyotuzunguka  katika utoaji wa huduma kwa manusura wa ukatili hususani kuwahudumia waathirika na utoaji wa vifaa ili kulinda ushahidi" alisema Mutajwaa

Kwa Upande wake Caspian Chouraya Mkurugenzi wa EGPAF kanda ya Afrika amesema shirika hilo linafanya kazi kuhakikisha kwamba watoto hawapati maambukizi ya virusi vya UKIMWI na ukatili wa aina yeyote ule huku akiishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi hiyo bega kwa bega.


"Madhumuni yetu ni kufanya kaz ili kuhakikisha watoto hawapati maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kuwalinda dhidi ya Ukatili na tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya kazi nasi bega kwa bega." Alisema Chouraya

Aidha mkuu wa wilaya ya Kiteto Remidius Mwema akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Manyara, amesisitiza kuendelea kuwepo kwa mashirikiano mazuri na taasisi za dini kwani kupitia taasisi hizo itasaidia kuendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wananchi.

"Tukiweza kuwaunganisha watu Hawa kwenye taasisi HIZI za dini itasaidia Sana kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye jamii." Alisema Mwema 

Huduma ya vituo vya mkono kwa mkono zinatolewa katika hospitali za serikali na vituo vya afya na serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali kama EGPAF imeendelea kutoa huduma katika vituo 27 vya mkono kwa mkono hapa nchini, na katika kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2024 nyumba 6 zimeanzishwa katika mikoa ya Arusha, Kigoma, Mara na Kilimanjaro.

Mwakilishi wa USAID AFYA YANGU Anne Maphy kutoka nchini Marekani, amesema wataendelea kushirikiana na nchi ya Tanzania katika kufadhili miradi mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo kuzuaia na kupinga vitendo vya Ukatili.

Pikipiki itakayotumika kusaidia huduma kwa watoa huduma kwenye kituo hicho ambacho kimeweka historia mpya mkoani Manyara.

Post a Comment

0 Comments