F Sillo awataka Viongozi wa dini kuiombea Serikali | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sillo awataka Viongozi wa dini kuiombea Serikali


Na John Walter-Babati

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa ngazi mbalimbali, kuanzia wenyeviti wa vijiji, vitongoji ,mitaa hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sillo amezungumza hayo alipoungana na wananchi wa kijiji cha Kwaraa, kata ya Endakiso, wilaya ya Babati mkoani Manyara, katika ibada ya mazishi ya mzee Abel Aweda (81) aliyefariki dunia Desemba 26, 2024.

Akizungumza katika ibada ya Mazishi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu kijijini hapo,  Mheshimiwa Sillo alitoa pole kwa familia ya marehemu na kuwataka wananchi kuishi kwa kushirikiana na kutenda mema. 

Aidha, Mheshimiwa Sillo aliwatakia wananchi wote heri na fanaka katika mwaka mpya wa 2025, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi.

Marehemu Mzee Abel Aweda, ambaye alikuwa mkulima na mfugaji mkubwa, ameacha watoto 27 (18 wa kike na 9 wa kiume), wajukuu 73, na vitukuu 32.

Mchungaji Marko Gillay wa Kanisa la Anglikana aliwaasa waombolezaji kumcha Mungu na kumwabudu wakati wote ili watakapoondoka duniani waendelee kuishi kiroho.

Diwani wa kata ya Endakiso, Hassan Omari Dodo, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Sillo kwa upendo mkubwa aliouonesha kwa kushiriki msiba huo. Aidha, diwani huyo alitumia nafasi hiyo kuomba serikali kuhakikisha kitongoji cha Sanya, kijiji cha Kwaraa, kinapatiwa huduma za umeme na maji.

Ibada hiyo ya mazishi ilikuwa na ujumbe wa mshikamano, upendo, na wito wa kuendelea kutenda mema kwa jamii.

"Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe."

Post a Comment

0 Comments