Na John Walter -Babati
Katika kuadhimisha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia inayoendelea kote ulimwenguni,Jamii imetakiwa kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya kikatili katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa SMAUJATA wilaya ya Babati, Ezekiel Tlanka alipokuwa akizungumza na wazazi wa Wanafunzi shule ya Msingi Komoto, walimu na Viongozi wa Kijiji cha Managhat kata ya Singe kwa nyakati tofauti, akitoa elimu juu ya umuhimu wa kupiga vita ukatili wa aina zote, ikiwemo ukatili wa kijinsia, wa watoto, na wa kisaikolojia, kingono ,kiuchumi kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuhakikisha usalama wa kila mtu katika jamii.
Tlanka aliwahimiza wananchi na Viongozi wa mitaa na Vijiji wilayani humo kushirikiana na mamlaka za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuripoti matukio ya ukatili na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Alisisitiza kuwa ukatili hauna nafasi katika jamii yenye maendeleo na amani, na kila mmoja ana jukumu la kushiriki katika kampeni hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Singe Martin Masumbuko Yahhi aliwasihi viongozi hao kuzingatia elimu wanayopewa na kutumia maarifa hayo kuleta mabadiliko chanya katika familia na jamii zao.
Naye Mwenyekiti wa SMAUJATA mkoa wa Manyara Philipo Sanka aliyeambatana na Mwenyekiti wa wilaya alisema kuwa kampeni hiyo inalenga sio tu kuelimisha, bali pia kubadili mitazamo na tabia zinazochangia ukatili.
Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili, ambayo ilianza rasmi Novemba 25, 2024, inatarajiwa kufikia kilele chake Desemba 10, 2024.
Hata hivyo Viongozi wa kijiji cha Managhat walionyesha mshikamano mkubwa na kuahidi kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii yao kwa kuhakikisha wanachukua hatua za kuzuia ukatili na kusaidia waathirika kupata msaada wa kisheria na kijamii.
Kaulimbiu ya kampeni hii mwaka 2024 ni "Baada ya Beijing+30: Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na wasichana"
0 Comments