F SMAUJATA Babati Watoa Elimu ya Ukatili kwa Wanafunzi wa Sekondari ya Singe | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

SMAUJATA Babati Watoa Elimu ya Ukatili kwa Wanafunzi wa Sekondari ya Singe

Na John Walter -Babati 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania  Tanzania (SMAUJATA) wilaya ya Babati, Ezekiel Tlanka, ameongoza juhudi za kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Singe kuhusu ukatili, madhara yake, na umuhimu wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili.

Katika semina hiyo, Tlanka alieleza kuwa ukatili kwa watoto na vijana una athari kubwa katika maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Aliwahimiza wanafunzi kutambua aina mbalimbali za ukatili, zikiwemo ukatili wa kijinsia, ukatili wa kimwili, na ukatili wa kihisia, na jinsi ya kujikinga dhidi yake.

“Ukatili ni adui wa maendeleo ya jamii, ni jukumu letu kama vijana na wananchi kupambana nao kwa nguvu zote,tunapaswa kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa pale tunaposhuhudia au kukumbwa na vitendo vya ukatili,” alisema Tlanka.

Akiwaelimisha wanafunzi, alisisitiza umuhimu wa kutumia njia rasmi za kuripoti ukatili, kama vile kutoa taarifa kwa walimu, viongozi wa shule, wazazi, au vyombo vya usalama. 

Pia, alitaja namba maalum za msaada ambazo wanafunzi wanaweza kuzitumia kuripoti matukio hayo kwa usalama na faragha ambazo ni 116.

SMAUJATA Babati imeahidi kuendelea kushirikiana na shule, jamii, na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa elimu dhidi ya ukatili inaendelea kutolewa na vitendo vya ukatili vinatokomezwa kabisa. 

Tlanka alihitimisha kwa kuwaasa wanafunzi kuwa mabalozi wa mabadiliko katika familia zao na jamii kwa ujumla.

Semina hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za SMAUJATA katika kulinda na kuimarisha ustawi wa watoto na vijana nchini Tanzania.


Post a Comment

0 Comments