Na John Walter -Babati
Waumini wa dini ya Kikristo wametakiwa kumcha Mungu kwa kutenda mema, kuwasaidia wenye uhitaji, kuwatembelea, na kuwalisha kama ishara ya upendo wa Kikristo.
Wito huu umetolewa na Mchungaji Isaya Jacob Lee katika ibada ya Noeli iliyofanyika leo Desemba 25, 2024, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Babati Mjini, Jimbo la Babati, Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Akihubiri mbele ya waumini waliohudhuria ibada hiyo, Mchungaji Lee amesisitiza umuhimu wa waumini kuishi kwa upendo hasa katika siku hii takatifu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Amesema kuwa Noeli ni wakati wa kujifunza kutoka kwa mfano wa Yesu Kristo, ambaye alikuja duniani kwa upendo na kujitoa kwa ajili ya wengine.
"Katika siku hii ya Noeli, tunapaswa kuonyesha upendo wa Kristo kwa vitendo kwa kuwaangalia wale walio na uhitaji, tuwasaidie, tuwatembelee, na kuwafariji, hili ndilo linalodhihirisha kumcha Mungu kwa matendo yetu mema," alisema Mchungaji Lee.
Ibada hiyo ya Noeli ilihudhuriwa na waumini wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Babati, ambapo walishiriki nyimbo za kumsifu Mungu, maombi, na ujumbe wa matumaini.
Waumini walihimizwa kuendelea kuishi kwa mshikamano na kusherehekea Noeli kwa amani na furaha, wakikumbuka maana halisi ya sikukuu hiyo.
Hata hivyo Mchungaji Lee alitoa wito kwa waumini wote kuendelea kuishi maisha ya utakatifu, uadilifu, na mshikamano wa Kikristo si tu wakati wa Noeli bali katika maisha yao ya kila siku.
0 Comments