F CCM Manyara yaunga mkono maazimio ya Mkutano mkuu Taifa. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

CCM Manyara yaunga mkono maazimio ya Mkutano mkuu Taifa.


Na John Walter -Manyara

Katika jitihada za kuonyesha mshikamano na kupongeza maamuzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu wagombea wake wa nafasi za juu za uongozi, matembezi ya amani yamefanyika leo Mjini Babati katika mkoa wa Manyara.

Tukio hili limeongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima, na kushirikisha wanachama na viongozi mbalimbali wa chama.

Matembezi haya yalilenga kuwaunga mkono wagombea waliopitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. 

Chama cha Mapinduzi kimeamua kumsimamisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea urais kwa Tanzania Bara, huku Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais. 

Kwa upande wa Zanzibar, chama kimeidhinisha Dkt. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya urais.

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Peter Toima alisema, "Maamuzi haya ni ya busara na yanaonyesha uimara wa chama chetu katika kuhakikisha tunawaletea Watanzania maendeleo endelevu, tunaamini wagombea wetu ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na umahiri."

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Taifa, Bi.Zainabu Shomari, alisisitiza kuwa hakuna chama kingine cha siasa chenye uwezo wa kuiondoa CCM madarakani.

 "CCM ni chama chenye historia, misingi imara, na kinaendelea kuonyesha dira ya maendeleo kwa Watanzania,tunapowapendekeza wagombea hawa, tunafanya hivyo kwa imani kubwa kuwa wataendelea kuimarisha uchumi na kuleta ustawi wa jamii," alisema.

Wanachama walioshiriki kwenye matembezi hayo, walibeba mabango yenye jumbe za kupongeza maamuzi ya chama na kuwaahidi wagombea hao ushirikiano wa dhati katika safari ya kuelekea ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema Chama cha Mapinduzi kimeonyesha nia ya kuendelea kuwa chombo cha kuaminika kwa Watanzania, huku kikiahidi kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wake.
Mwisho

Picha mbalimbali kwenye matembezi leo Mjini Babati kuunga mkono maazimio ya Mkutano mkuu wa CCM Taifa.


























Post a Comment

0 Comments