MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imetoa mwito kwa benki za biashara,benki za wananchi na benki za maendeleo kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji kama ambavyo Benki ya DCB imetumia fursa hiyo kwa kuuza hisa stahiki, na hatimaye kupata fedha za kukuza na kuendeleza biashara na kugharamia shughuli za maendeleo.
Akizungumza leo Januari 10,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hisa stahiki za Benki ya DCB katika Soko la Hisa Dar es Salaam ,Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA CPA Nicodemua Mkama amesema ni vema benki mbalimbali zikaona umuhimu wa kutumia fursa hizo ili kukuza na kuimarisha biashara zao.
Kuhusu kuorodheshwa kwa hisa stahiki za Benki ya DCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam ,CPA Mkama amesema hatua hiyo ni muhimu kwa sekta ya fedha, kwani imewezesha utekelezaji wa matakwa ya sheria kwa benki za biashara, benki za wananchi pamoja na benki za maendeleo kutimiza matakwa ya sheria inayosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha ili kujiendesha kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo.
“Oktoba 11, 2024, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) iliidhinisha Waraka wa Matarajio wa benki ya DCB kuuza Hisa Stahiki zenye thamani ya shilingi bilioni 10.74.Idhini ilitolewa na CMSA baada ya benki ya DCB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hisa Stahiki.
“Kwa mantiki hii mauzo ya Hisa Stahiki za benki ya DCB yamefanyika kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji.Mauzo ya Hisa Stahiki za Benki ya DCB yalizinduliwa rasmi Novemba 11,2024 na kufungwa Desemba 6, 2024, ambapo maombi yenye thamani ya shilingi bilioni 10.74 yamepokelewa kama ilivyotarajiwa sawa na mafanikio ya asilimia 100.
“Fedha zilizopatikana kupitia mauzo haya zitatumika kutekeleza mikakati ya benki ya DCB ya kukuza na kuendeleza biashara, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali. Mauzo haya yataiwezesha benki ya DCB kutimiza malengo yake ya kimkakati ya kukuza thamani ya uwekezaji kwa wanahisa wake katika benki.”
CPA Mkama amesema katika mauzo ya Hisa Stahiki za benki ya DCB, asilimia 50.18 ya wawekezaji walioshiriki ni wawekezaji mmoja mmoja (Retail Investors) na asilimia 49.82 ya wawekezaji ni Kampuni na Taasisi.Aidha, asilimia 100 ya wawekezaji ni wawekezaji wa ndani.
Amefafanua mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi, na shirikishi ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi Madhubuti wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesisitiza hivyo kuna kila sababu ya kuipongeza Benki ya DCB na wadau wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio hayo na kuongeza mauzo hayo pia ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza mikakati ya kukuza na kuendeleza biashara; na kugharamia shughuli za maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.
Aidha, mafanikio hayo yanawezesha utekelezaji wa malengo ya Jukwaa la Uthabiti wa Sekta ya Fedha ya kuendeleza na kulinda uthabiti wa sekta ya Fedha, ambapo benki inapokuwa na mtaji wa kutosha unaokidhi matakwa ya kisheria huwezesha sekta ya fedha kuwa imara na thabiti.
“Kuorodheshwa kwa Hisa Stahiki za benki ya DCB kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kunawapatia fursa wawekezaji kuuza hisa zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine.Uorodheshwaji wa hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hisa zao na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hisa hizo ambapo wawekazaji hao watapata gawio kama faida itokanayo na uwekezaji huo.
“Vile vile, uorodheshwaji wa kampuni katika soko la hisaunaongeza Utawala Bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa zaidi za uwekezaji. Hiyo inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji,”amesema.
Pamoja na hayo amesema Masoko ya mitaji Tanzania yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla, ambapo, benki na Taasisi za Fedha kama vile Benki ya NMB, CRDB, Exim, Azania na Standard Chartered
Pia kuna benki za nje kama Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Benki ya Maendeleo ya Biashara Afrika (PTA-TADB) ambazo zimekuwa zikitumia masoko ya mitaji hapa nchini kuongeza rasilimali fedha, hivyo kuimarisha uwezo wa benki na taasisi hizo kutoa huduma kwa wateja katika sekta ya umma na binafsi
0 Comments