Na Walter -Manyara
Jiji la Dodoma limepambwa na pilikapilika nyingi kuelekea Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaotarajiwa kufanyika Januari 18 na 19 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Tukio hili muhimu litakuwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo umekuwa kivutio kikubwa si tu kwa wanachama wa CCM, bali pia kwa wakazi wa Dodoma.
Wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza kuwasili jijini humo, huku misafara mikubwa ya magari yenye rangi za bendera za chama ikionekana barabarani, ikionyesha umoja na mshikamano wa chama hicho.
Mbali na vikao vya kisiasa, tukio hilo limepangwa kuwa la kipekee kwa burudani, ambapo wasanii maarufu nchini kama Diamond Platnumz, Ali Kiba, Harmonize, na wengine wengi wanatarajiwa kutumbuiza.
Burudani hizi zinatarajiwa kuvutia watu wengi zaidi, wakitoa ladha ya kipekee katika tukio hilo kubwa.
Kwa wakazi wa Dodoma, hii ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara wa chakula, hoteli, usafiri, na huduma nyinginezo za kijamii. Wengi wao wamejipanga kuhudumia idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kufurika jijini humo kwa siku hizi mbili za mkutano.
Dodoma kwa sasa imekuwa kitovu cha siasa na burudani, ikidhihirisha nafasi yake kama makao makuu ya nchi na nguzo ya shughuli za kitaifa.
0 Comments