F Gekul akabidhi mabati 90 Ujenzi nyumba za watumishi CCM Mjini Babati | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Gekul akabidhi mabati 90 Ujenzi nyumba za watumishi CCM Mjini Babati



Na John Walter-Babati 

Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, amekabidhi mabati 90 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba za watumishi wa Jumuiya ya Wazazi mtaa wa Sinai, kata ya Maisaka.

Msaada huo unalenga kuhakikisha nyumba hizo zinakamilika na kuanza kutumika kwa manufaa ya watumishi wa jumuiya hiyo.

Aidha, aliwataka viongozi wa jumuiya hiyo kukemea maovu katika jamii, hasa vitendo vya ukatili wa kijinsia, mmomonyoko wa maadili, na migogoro ya kifamilia.

“Vitendo vya ukatili vinaacha makovu makubwa kwa waathirika, hasa watoto yatima na familia kwa ujumla, Jumuiya hii inapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea mambo haya ambayo yanachafua sifa ya wilaya na mkoa wetu wa Manyara, CCM haipendezwi na matukio haya, hivyo ni jukumu letu kama wanajumuiya kuisaidia jamii kuondokana na changamoto hizi,” alisema Gekul.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Babati Mjini, Nassoro Msaka, alimpongeza Mbunge Gekul kwa msaada huo ambao utafanikisha kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hizo. 

Aliahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na kushughulikia changamoto za ndani ya jumuiya, ikiwa ni pamoja na kupambana na fitina na chuki miongoni mwa wanajumuiya.

“Jumuiya yetu itahakikisha inatoa malezi bora kwa vijana, inakemea wachonganishi, na inasaidia jamii kwa ujumla, Tunapokea msaada huu kwa shukrani kubwa na tutahakikisha tunautumia ipasavyo kwa maendeleo ya jumuiya,” alisema Nassoro.

Jumuiya ya Wazazi ni nguzo muhimu ya CCM na inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwahamasisha wananchi, kuimarisha mshikamano.

Post a Comment

0 Comments