F Kituo cha Afya Bashnet chazinduliwa rasmi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kituo cha Afya Bashnet chazinduliwa rasmi



Na John Walter -Babati

Waziri wa nchi, ofisi ya Rais mipango na uwekezaji , Prof. Kitila Mkumbo, amezindua rasmi Kituo cha Afya cha Bashnet kilichopo wilayani Babati. Kituo hiki kilianza kutoa huduma za afya kwa kina mama, ikiwemo huduma za kujifungua, ambapo tayari akina mama 26 wamejifungua salama tangu kuanza kwa huduma hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo januari 4,2025, Waziri Mkumbo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtuma kufungua kituo hicho kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020 akiwa mgombea mwenza awamu ya tano chini ya Hayati Dkt John Pombe Magufuli.

Kituo hicho kimejengwa na Serikali kufuatia maombi ya wananchi wa Bashnet kupitia kwa Diwani wao, Jovitha Mandoo. Katika tukio la kihistoria, diwani huyo alipiga magoti na kugaragaa mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akiwa mgombea mwenza mwaka 2020, akiomba kituo cha afya kutokana na changamoto kubwa za huduma za matibabu zilizokuwa zikiwakumba wananchi wa eneo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alitoa shukrani zake kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi kwa kutekeleza miradi mikubwa jimboni humo, hususan katika sekta ya afya.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Babati, Madama Hosea, ameeleza kuwa  shilingi milioni 632 zimetumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya, ambacho sasa kinatoa huduma muhimu kwa wakazi wa Bashnet na maeneo jirani tangu Desemba 1, 2024.

Wananchi wa Bashnet wamepongeza juhudi za Serikali na kueleza kuwa kituo hiki ni mkombozi mkubwa kwao, hasa katika kupunguza changamoto za kupata huduma za afya umbali mrefu.


Post a Comment

0 Comments