Na John Walter -Manyara
Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wassira, ameeleza kuwa uteuzi wake ni matokeo ya uongozi wa Mungu kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Wassira alitoa shukrani zake kwa Rais Dkt. Samia kwa imani kubwa aliyomwonyesha katika nafasi hiyo.
Katika hotuba yake baada ya uteuzi, Wassira aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kwa kumpigia kura 1,910.
Amebainisha kuwa zaidi ya nusu ya wajumbe hao anawafahamu vyema na tayari amewahi kuzungumza nao kupitia simu.
Aidha, aliwapongeza hata wale wachache waliokuwa na mashaka juu yake, akisema kuwa hakuwahi kushika nafasi hiyo kabla, lakini sasa ana nia ya dhati ya kuwatumikia kwa uadilifu.
Wassira ameeleza kuwa jukumu lake kuu ni kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kuwa mafanikio ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni hatua kubwa, na sasa chama hicho kinajiandaa kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumzia maendeleo yaliyofikiwa, Wassira amesema serikali ya CCM haina deni kwa wananchi kwa kuwa imefanikiwa kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali, na kuboresha miundombinu ya barabara kote nchini.
Wassira aliomba ushirikiano kutoka kwa wanachama wa CCM na hata wale ambao si wanachama akisisitiza kuwa chama hicho ni cha amani na ushirikiano, na kwamba ana azma ya kuendeleza maridhiano na mshikamano katika jamii.
Akiwa ameanza majukumu yake mapya, Wassira aliahidi kushirikiana na wanachama wote wa CCM kuhakikisha amani na maendeleo vinaendelea kuwa nguzo za msingi za chama hicho.
0 Comments