Shule ya Sekondari Ayalagaya, iliyopo katika wilaya ya Babati, mkoa wa Manyara, imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2024, yaliyotangazwa rasmi tarehe 23 Januari 2025.
Katika matokeo hayo, shule hiyo imefanya mabadiliko makubwa kwa kuondoa daraja la nne kabisa, huku ikijivunia madaraja ya juu.
Shule hiyo imepata madaraja ya kwanza 80, daraja la pili 65, na daraja la tatu 2.
Mafanikio haya yameifanya shule ya Ayalagaya kuwa mfano wa kuigwa katika shule za serikali za mkoa wa Manyara.
Kwa upande mwingine, shule ya Dareda, ambayo hapo awali ilijulikana kwa kufanya vizuri zaidi, imepata madaraja ya kwanza 48, daraja la pili 92, daraja la tatu 78, na daraja la nne 20.
Hali hii imeonyesha ushindani mkubwa baina ya shule hizo mbili, huku Ayalagaya ikichukua nafasi ya juu zaidi mwaka huu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karim Foundation Tanzania, Shau Erro Ae, ambaye taasisi yake imetoa mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa Ayalagaya, amepongeza walimu, wazazi, na wanafunzi kwa jitihada zao kubwa.
Amesisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya pande zote zinazohusika.
“Mazingira rafiki ya kujifunzia ni msingi wa mafanikio ya wanafunzi wetu,tunajivunia kuona jitihada zetu zikizaa matunda,” alisema Mkurugenzi huyo.
Shule ya Sekondari Ayalagaya sasa imekuwa mfano wa kuigwa, ikionyesha jinsi uwekezaji katika elimu na mshikamano wa jamii unaweza kuleta matokeo chanya.
0 Comments