Na John Walter -Dodoma
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), chini ya uongozi wa Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, limeadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya shughuli ya kupanda miti ya vivuli na matunda.
Tukio hili limefanyika katika ushoroba wa Bolisa, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma, kama sehemu ya uzinduzi wa mradi wa "Dkt. Samia Suluhu Green Highway ikiwa na kauli mbiu: "Tumpambe kwa Maua ya Kijani"
Shughuli hiyo imelenga kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuhifadhi mazingira, kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kukuza maendeleo endelevu.
Kupitia kauli mbiu ya "Tumpambe kwa maua ya kijani," BAKWATA imehamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya watu.
Miongoni mwa miti iliyopandwa ni "Mti wa Mama," uliopandwa kama ishara ya heshima na shukrani kwa mchango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya nchi.
Ikumbukwe kuwa upandaji wa miti siyo tu jukumu la kijamii bali pia ni sehemu ya ibada, hata maneno ya Mtume Muhammad (SAW) yanasema
"Kiyama kitakapofika, ukiwa na mche wa mti mkononi, panda kwanza."
Mradi huo wa kijani, unaojulikana kama "Dkt. Samia Suluhu Green Highway," ni mpango wa kimkakati unaolenga kuimarisha ushoroba wa Bolisa kwa kupanda miti yenye manufaa kwa mazingira na jamii.
Miti iliyopandwa ya vivuli na matunda itasaidia kupunguza joto, kuboresha hewa safi, na kutoa chakula kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kwa ujumla, shughuli hii ni mfano mzuri wa mshikamano wa kitaifa na mchango wa taasisi za kidini katika maendeleo endelevu ya Tanzania.
0 Comments