F Wananchi wa Arri Wanufaika na Mradi Mkubwa wa Maji | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wananchi wa Arri Wanufaika na Mradi Mkubwa wa Maji



Na John Walter -Babati

Zaidi ya wananchi 3,000 wa Kata ya Arri, Wilaya ya Babati mkoani Manyara wameanza kunufaika na mradi mkubwa wa maji uliojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa ufadhili wa Shirika la Karim Foundation kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amezindua rasmi mradi huo leo januari 4,2025 na kuwapongeza wahisani kwa upendo wao na jitihada za kuchangia maendeleo ya jamii. 

Waziri Mkumbo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani, akisema miradi kama hiyo ni hatua kubwa kuelekea kufanikisha lengo hilo.

Mkurugenzi wa Karim Foundation Tanzania, Shau Erro Ae, ameeleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2.482 zimetumika katika mradi huo, huku wananchi wakichangia shilingi milioni 128 kwa nguvu kazi, ikiwemo kuchimba mitaro na shughuli nyingine za ujenzi. 

"Kwa sasa, hakuna mwananchi anayefuata maji umbali wa zaidi ya mita 400, hali ambayo imeboresha maisha ya wakazi wa Arri" alisema Shau

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, amesema mradi huo umeongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya ya Babati Vijijini kufikia asilimia 83.

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Daniel Sillo, amewashukuru wahisani na Serikali kwa jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji, akisisitiza kuwa mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa jamii ya Arri.

Wananchi wa Kata ya Arri wameeleza furaha yao kwa mradi huo, wakisema kuwa utapunguza changamoto za muda mrefu za upatikanaji wa maji safi na salama.

Post a Comment

0 Comments