F Waziri Kitila Mkumbo apongeza uwekezaji wa Mulokozi. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Waziri Kitila Mkumbo apongeza uwekezaji wa Mulokozi.



Na John Walter -Babati

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amempongeza mwekezaji David Mulokozi kwa uwekezaji wake kupitia Kampuni ya Mati Super Brands LTD, akiwataka Watanzania wengine kuiga mfano huo kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali ndani ya nchi. 

Waziri Mkumbo amesisitiza kuwa wawekezaji sio lazima watoke nje ya nchi na kwamba Watanzania wana nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akiwa Mjini Babati, Manyara, Waziri Mkumbo amesema kiwanda hicho, ambacho kimeajiri Watanzania 269, kimechangia ukuaji wa uchumi na kuupendezesha mji wa Babati. 

Ametoa wito kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha wawekezaji wa aina hiyo wanapewa kipaumbele na wasikutane na vikwazo vyovyote katika shughuli zao za uwekezaji.

“Serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya uwekezaji ili wawekezaji wasipate changamoto zisizo za lazima, pamoja na kuwa na matumizi ya mitambo ya kisasa, tunapaswa kuzingatia ajira kwa vijana ili kuimarisha usalama wa nchi,” alisema Waziri Mkumbo.

Ameongeza kuwa taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC) zina jukumu la kudhibiti bidhaa bandia na biashara zinazokiuka taratibu rasmi ili kulinda ukusanyaji wa kodi na ubora wa bidhaa. 

Waziri Mkumbo pia amebainisha kuwa serikali inafanya mabadiliko ya sheria za uwekezaji ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mati Super Brands LTD, David Mulokozi, ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni wazalishaji wa pombe kali zisizo na ubora, hali inayoharibu taswira ya bidhaa zao.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kulipa shilingi bilioni 8 kama kodi kwa serikali mwaka 2024, na inalenga kufikia bilioni 12 katika siku zijazo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mariam Muhaj, alifafanua kuwa Waziri Mkumbo alitembelea na kuzindua miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 11.6 akiwa mkoani humo.

Post a Comment

0 Comments