Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, mipango na uwekezaji, Kitila Mkumbo, amezindua rasmi Kituo cha Afya Sigino kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara.
Ujenzi wa kituo hicho umegharimu Shilingi milioni 434, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha huduma za afya nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo januari 4,2025, Waziri Mkumbo amesema kuwa lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa urahisi na uhakika, kwa wananchi wa maeneo ya mijini na vijijini.
Amempongeza Diwani wa eneo hilo pamoja na Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mheshimiwa Paulina Gekul, kwa juhudi zao za kuhakikisha wananchi wa Sigino wanapata kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Paulina Gekul amesema kuwa kituo hicho cha afya ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi wa Sigino, na sasa kina mama wa eneo hilo wanaweza kupata huduma za afya karibu zaidi.
Hata hivyo, Gekul amebainisha kuwa kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chumba cha upasuaji, na hivyo ameomba serikali kusaidia kukamilisha huduma hiyo muhimu.
Uzinduzi wa kituo hicho ni moja ya hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Sigino na maeneo jirani, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kuimarisha ustawi wa jamii kwa vitendo.
0 Comments