MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana imetoa pongezi kwa Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa benki ya CRDB kwa kutupatia furaha kubwa katika sekta ya masoko ya mitaji, kwa kuwa mauzo ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia kwa kupata mafanikio ya asilimia 215.4, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 323.09 kimepatikana ikilinganishwa na Sh.bilioni 150 zilizopangwa kupatikana.

Kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, kumeongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 38.59 na kufikia Shilingi trilioni 1.16, kutoka Shilingi bilioni 837.31.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus Mkama leo Februari 18,2025 jijini Dar es Salaam na wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya miundombinu ya Samia katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

“Mafanikio haya yana maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha. Kwanza, inaonesha imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya CRDB na masoko ya mitaji. Pia masoko ya mitaji hapa nchini yamekuwa kivutio na kutoa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji mmoja mmoja; Taasisi; wawekezaji wa ndani; na wawekezaji wa kimataifa.

“Tatu, kutokana na mazingira wezeshi katika masoko ya mitaji, bidhaa mpya na bunifu zinatolewa, hivyo kuwezesha Kampuni, Taasisi na benki kama CRDB kupata fedha za kuendeleza na kukuza biashara; na kugharamia shughuli za maendeleo, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara zilizo chini ya TARURA zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

“Hivyo, tuna kila sababu za kuipongeza Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa benki ya CRDB; TARURA; pamoja na taasisi na wataalamu katika masoko ya mitaji waliowezesha kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Uuzaji wa Hatifungani hii kwa umma.”


Ameongeza mafanikio hayo ni uthibitisho wa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan huku akifafanua lengo kuu la Hatifungani hiyo ni kuwawezesha wakandarasi wa ndani ambao wanafanya kazi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa na uwezo wa kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini hapa nchini.

CPA Mkama amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

Pia amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zilizopatikana zitatumika kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi; na wananchi waliowekeza katika hatifungani hiyo watalipwa riba, hivyo kuinua vipato vyao.
“Tunaipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao umewezesha CRDB kushirikiana na TARURA kutoa Hatifungani hii, hivyo kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuinua vipato vyao; na kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi.

“Kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kunawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine.”

Aidha amesema uorodheshwaji wa hatifungani katika Soko la Hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hatifungani zao na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo wawekazaji hao watapata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.


Ameongeza uorodheshwaji wa hatifungani katika soko la hisa unaongeza Utawala Bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa zaidi za uwekezaji.Hiyo inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji.

Pamoja na hayo CPA Mkama amesema CRDB ni miongoni mwa kampuni ambazo zinatumia vizuri fursa katika masoko ya mitaji na kuongeza benki hiyo imeuza hisa kwa umma na imeorodheshwa katika soko la hisa.

Pia benki hiyo imepata rasilimali fedha za zaidi ya Sh.bilioni 500 zilizotokana na mauzo ya bidhaa mbalimbali katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na Hatifungani ya Kijani na Hatifungani ya Miundombinu.CRDB ina leseni nne kutoka CMSA za kutoa huduma katika masoko ya mitaji.

Amesema kutokana na mafanikio hayo Benki ya CRDB inatekeleza mikakati ambayo inaleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki, wanahisana masoko ya mitaji. Mathalani, Bei ya hisa za Benki ya CRDB imeongezeka kwa asilimia 366.7 kutoka Sh. 150 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa katika soko la awali, hadi Sh.700 kwa hisa, kwa Februari 17, 2025.

Amefafanua kama Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ilitoa idhini kwa benki ya CRDB kufanya mauzo ya Hatifungani ya Miundombinu ya Samia yenye thamani ya Sh.bilioni 150, kuanzia Novemba 29, 2024 hadi Januari 17,2025. Idhini hiyo ilitolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inayohusu utoaji wa Hatifungani kwa umma.

Aidha ametoa mwito kwa Benki zingine za Biashara, Taasisi za Fedha, kampuni binafsi, Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji kama ambavyo Benki ya CRDB na TARURA wametumia fursa ya kupata shilingi bilioni 323.09 kupitia masoko ya mitaji kwa kuuza hatifungani.