F ECLAT na Upendo Kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana Simanjiro. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

ECLAT na Upendo Kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana Simanjiro.


Na John Walter -Simanjiro 

Shirika la ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION kwa kushirikiana na Upendo Association limepanga kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya bweni katika Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara. 

Shule hiyo itakuwa na madarasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, ikiwa ni hatua kubwa katika kuboresha elimu kwa wasichana katika eneo hilo.

Meneja Miradi wa ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION, Bakir Angalia, amethibitisha kuwa shule hiyo itakuwa ya ghorofa na inatarajiwa kugharimu mabilioni ya fedha hadi kukamilika kwake. 

Amebainisha kuwa ujenzi wake unatarajiwa kuanza kati ya mwezi Machi na Aprili mwaka huu, na ifikapo tarehe 23 Agosti 2026, jiwe la msingi litawekwa huku majengo mengine yakiwa tayari kwa matumizi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terati, Kone Medukenya, ameweka wazi kuwa tayari wameketi vikao na kutenga eneo lenye ukubwa wa hekari 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo katika kitongoji cha Ormanie. 

Mkurugenzi wa ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION, Peter Toima, ametangaza kuwa shule hiyo itaitwa Tukuta Girl’s Secondary School, jina la Kimaasai lenye maana ya "upepo mwanana," kutokana na eneo hilo kuwa na upepo mwingi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa shirika la Upendo Association kutoka Ujerumani, Dr. Fred Heimbach, ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waanze masomo Januari 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Simanjiro, Gracian Makotha, pamoja na timu ya wilaya walitembelea eneo la ujenzi na kutoa ahadi ya ushirikiano kwa wafadhili katika kila hatua ya mradi huo.

Ameishukuru ECLAT DEVELOPMENT FOUNDATION kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri hiyo, akisema kuwa hii ni njia muhimu ya kuisaidia serikali kuhudumia wananchi kwa uzalendo mkubwa.

Mkurugenzi huyo pia amewataka wananchi kutumia fursa ya ujenzi wa shule hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowapatia kipato, kwani ajira nyingi zinatarajiwa kupatikana wakati wa ujenzi.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na Diwani wa kata hiyo ya Terati Baraka Kanunga amesema watasimamia na kuwahimiza RUWASA na TANESCO kupeleka huduma haraka katika eneo hilo.

Masharti yaliyotolewa na mfadhili wa shule hiyo ni kwamba kijiji kipande miti 1,000 kuzunguka eneo hilo, na tayari kijiji kimethibitisha kuridhia masharti hayo.

Hii itakuwa shule ya pili ya wasichana katika mkoa huu baada ya ile iliyojengwa na serikali mjini Babati.

Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwa wasichana wa Simanjiro, Manyara, na Tanzania kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments