F Mbunge Gekul apongeza hatua ya CCM kuongeza wapiga Kura. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mbunge Gekul apongeza hatua ya CCM kuongeza wapiga Kura.

Na John Walter -Babati

Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mheshimiwa Paulina Gekul, amepongeza hatua ya kuongeza idadi ya wapiga kura wa ndani ya chama, akieleza kuwa hatua hiyo itaweka ugumu kwa watu kutumia fedha zao kununua uongozi. 

Akizungumza na viongozi wa matawi ya Logia, Bonga, na Himiti, Mhe. Gekul amesema kuwa ni mpango mzuri wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kuwa rushwa inaondolewa katika chaguzi za ndani ya chama na zile za uongozi wa kisiasa.

Amesema kuwa kwa kuwa na idadi kubwa ya wajumbe, itakuwa vigumu kwa wagombea kuhonga wapiga kura, hivyo kupunguza changamoto ya rushwa.

Mhe. Gekul pia amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maamuzi hayo ambayo amesema ni ya msingi katika kuimarisha demokrasia ndani ya chama.

Akiwahutubia viongozi hao, amewataka wajumbe kuwa waadilifu na waaminifu kwa kuwachagua wagombea wenye nia ya kuwatumikia wananchi, badala ya kuchagua viongozi kwa maslahi binafsi au kwa sababu ya fedha zao.

Jimbo la Babati Mjini, ambalo awali lilikuwa na takribani wapiga kura wa ndani 500, sasa linakadiriwa kuwa na zaidi ya 6,000, hatua inayotajwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha demokrasia ndani ya chama na kupunguza mianya ya rushwa kwenye chaguzi.


Post a Comment

0 Comments