F Mwanafunzi atoroshwa, DC Babati aingilia kati | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mwanafunzi atoroshwa, DC Babati aingilia kati


Na John Walter -Babati
Mama mmoja, Regina Sultan, amelalamika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, akidai kuwa binti yake wa kidato cha nne ametoroshwa na bibi yake aitwaye Scolastica Basso, na kupelekwa kufanya kazi za ndani katika eneo lisilojulikana.

Kwa mujibu wa Regina, binti yake hajaonekana nyumbani tangu Januari 2025.

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mara ya mwisho alionekana katika eneo la Masakta, Wilaya ya Hanang’, lakini inadaiwa amehamishiwa sehemu nyingine.

Mkuu wa Wilaya, Emmanuela Kaganda, ameonya vikali wazazi na walezi wanaotorosha watoto wao na kuwazuia kupata elimu.

Kaganda amesisitiza kuwa ni haki ya kila mtoto kupata elimu ili waweze kuwa viongozi wa baadaye wa taifa.

Kutokana na tukio hilo, ameagiza mama huyo, Scolastica Basso, akamatwe na kushikiliwa na polisi hadi atakapotoa taarifa za alipo binti huyo ili arejee shule kuendelea na masomo yake katika Shule ya Sekondari Qameyu.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Gawal, DC Kaganda alikutana na kisa kingine cha mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 ambaye hajaanza shule. 

Mkuu huyo wa wilaya aliguswa na hali ya mtoto huyo na kutoa fedha kwa ajili ya sare za shule na vifaa vingine, huku dada yake akipewa jukumu la kuhakikisha mtoto huyo anaanza masomo mara moja.

Aidha amewataka Wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu wazazi wanaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule. 

Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati,  Gloriah Yusto Shilly, akizungumza kwa niaba ya afisa elimu Msingi wilaya, amemuelekeza Afisa Elimu Kata ya Qameyu kuhakikisha mtoto huyo anaanza shule kabla ya Februari 26, kabla ya kufungwa kwa utaratibu wa usajili.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto wote na kutoa wito kwa jamii kushirikiana kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya kusoma.

Post a Comment

0 Comments