F Mwannchi Babati atekwa mchana kweupe | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mwannchi Babati atekwa mchana kweupe



Na John Walter -Babati 

Familia ya mfanyabiashara wa mafuta ya kula wilayani Babati, mkoani Manyara, Bashiru Hamis, wanadai kuwa ndugu yao alitekwa na watu wasiojulikana waliodai kuwa wateja wake. 

Kwa mujibu wa taarifa za familia, Bashiru alipigiwa simu na watu hao wakijifanya wateja wa mafuta ya kula, na walipokutana naye, walimlazimisha kuingia kwenye gari na kutoweka naye kusikojulikana. 

Dereva wa bodaboda aliyembeba Bashiru siku ya tukio amesema kuwa mfanyabiashara huyo alipokea simu kutoka kwa watu waliodai kuwa ni wateja, wakimtaka awapelekee mafuta ya kupikia jumla ya lita 40. 

Hata hivyo, alipofika eneo walilokubaliana, alitekwa na kuingizwa kwa nguvu kwenye gari na watu hao. 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kija Mkoyi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa jeshi la polisi linafanya ufuatiliaji wa kina ili kubaini walipo Bashiru na kuwakamata wahusika wa utekaji huo. 

Familia ya Bashiru imeiomba serikali na jeshi la polisi kuongeza juhudi katika kumtafuta ndugu yao ili aweze kupatikana na kurejea kwenye shughuli zake za kila siku. 

Pia, wamewataka wananchi wenye taarifa zozote kuhusu tukio hili kuzifikisha kwa vyombo vya usalama ili kusaidia katika uchunguzi na kumrudisha Bashiru salama.

Post a Comment

0 Comments