Na John Walter -Manyara
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Peter Toima Kiroya, amewaonya wanasiasa wanaotumia majukwaa ya kijamii kusambaza chuki na kutoa taarifa za uongo zinazoweza kuvuruga umoja wa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya shukrani kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Loiborsoit A, Lengay Lemonji, Mheshimiwa Toima ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa muda wa kufanya siasa bado, hivyo kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Toima alishangazwa na kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuhudhuria shughuli hiyo bila hata kualikwa na kuanza kuzungumza mambo ambayo yalikuwa nje ya lengo la sherehe.
“Wenyeviti wa mitaa, vijiji, vitongoji na mitaa wanapaswa kufanya kazi kwa weledi kwa mujibu wa sheria za nchi na Ilani ya CCM, Wanatakiwa kuwatumikia wananchi kwa upendo, kutatua changamoto zao au kuzifikisha sehemu husika badala ya kuendekeza migogoro,” alisema Mheshimiwa Toima.
Aliwasihi viongozi na wananchi kumtanguliza Mungu katika kila jambo na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Pia alisisitiza kuwa wakati wa uchaguzi utakapowadia, wananchi wamchague kwa kura nyingi Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Toima alionya vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaogeuza hafla za kijamii kuwa majukwaa ya kisiasa na kutumia fursa hizo kujipatia umaarufu au kujigamba.
Alisema hali hiyo huleta taharuki na migongano isiyo ya lazima ndani ya jamii, kinyume na dhamira njema ya wenye sherehe.
Aidha, alieleza kuwa wanasiasa wanapaswa kutumia majukwaa kama haya kuhamasisha mshikamano wa wananchi na kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kupandikiza chuki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Loiborsoit A, Lengay Lemonji, aliwashukuru wananchi kwa kumuamini na kumchagua kwa kura nyingi.
Pia alimshukuru mgeni rasmi kwa kuhudhuria hafla hiyo.
Wanakijiji wa Loiborsoit A walimpongeza mwenyekiti wao kwa kumpatia zawadi mbalimbali kama ishara ya kuthamini mchango wake katika maendeleo ya kijiji hicho.
0 Comments