F Sillo kwenye miaka 48 ya CCM Jimboni kwake,. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sillo kwenye miaka 48 ya CCM Jimboni kwake,.

Na John Walter -Babati

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, na Mbunge wa Babati Vijijini Daniel Sillo ameongoza wananchi wa Kata ya Secheda katika kusherehekea maadhimisho ya miaka 48 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika katika kijiji cha Luxmanda leo Februari 1, 2025, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano, Amani na Upendo kwa maendeleo endelevu ya Chama hicho.

Naibu Waziri alisisitiza kuwa CCM imeendelea kuwa nguzo imara ya maendeleo ya Taifa tangu kuasisiwa kwake kwa kujenga misingi ya upendo, amani na utulivu nchini.

Akiwa katika hafla hiyo, Mhe. Sillo alikagua jengo jipya la Zahanati ya Luxmanda huku akiwapongeza wananchi kwa jitihada zao katika kuboresha Sekta ya Afya ambapo alibainisha kuwa alihamasika kuunga mkono juhudi za Zahanati hiyo kwa kuchangia bati 117 kwa ajili ya ujenzi huo.

 Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha Shilingi Milioni 50 zilizosaidia kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo.

Aidha kwa upande wa Sekta ya Elimu, Mhe. Sillo alieleza kuwa Serikali katika miaka Minne imeongeza Shule tatu mpya za Sekondari ikiwa ni kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora katika mazingira rafiki.

Akizungumzia sekta ya Nishati, alisema kuwa kila kijiji katika Kata ya Secheda kimepata umeme isipokuwa baadhi ya vitongoji ambavyo Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha vinapatiwa huduma hiyo muhimu

Naibu Waziri alihitimisha hafla hiyo kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha Sekta zote za maendeleo, ikiwa ni pamoja na Afya, Elimu, miundombinu ya barabarani pamoja na Mawasiliano, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments