Na John Walter -Babati
Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Babati Mjini, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Eva Makilagi Luoga, umeadhimisha miaka 48 tangu kuzaliwa kwa CCM kwa kufanya shughuli za kijamii katika Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Manyara.
Katika maadhimisho hayo, UWT Babati Mjini, wakiwa wameambatana na Kamati ya Utekelezaji, walipanda miti katika mazingira ya shule hiyo kama sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuhamasisha upandaji wa miti kwa maendeleo endelevu.
Aidha Mheshimiwa Luoga alikabidhi jumla ya taulo za kike 250 zilitolewa kwa wanafunzi wa shule hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wasichana kupata elimu bila vikwazo vya ukosefu wa taulo za kujisitiri.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Eva Makilagi Luoga alisisitiza umuhimu wa elimu kwa wasichana na kuwaasa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufanikisha ndoto zao na kuwa viongozi wa baadaye.
Pia, Umoja wa Wanawake wa CCM Babati Mjini uliunga mkono azimio la Mkutano Mkuu la kuteua jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, kuwa wagombea pekee wa nafasi ya Urais kupitia CCM katika uchaguzi ujao.
UWT Babati Mjini ilimpongeza Rais Samia kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Manyara, hatua inayosaidia kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa kike.
Maadhimisho haya yalifanyika kwa mafanikio makubwa, yakionyesha mshikamano wa UWT katika kuunga mkono maendeleo ya jamii na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za chama na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Picha mbalimbali za UWT Babati Mjini kwenye maadhimisho ya miaka 48 ya chama cha Mapinduzi.
0 Comments