F Wananchi wa Ngapapa Gizani kwa miezi miwili | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wananchi wa Ngapapa Gizani kwa miezi miwili


Na John Walter -Kiteto
Wananchi wa Kijiji cha Ngapapa, wilayani Kiteto, bado wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa huduma ya umeme kwa zaidi ya miezi miwili, hali inayowaathiri katika shughuli zao za kila siku, zikiwemo biashara, elimu, na huduma za kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Kiteto, tatizo hilo limesababishwa na hitilafu kwenye moja ya transfoma inayohudumia kijiji hicho. TANESCO imesema tayari wameshawasilisha taarifa kwa uongozi wa mkoa kwa hatua zaidi, lakini hadi sasa tatizo bado halijapatiwa suluhisho.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema, ametoa maagizo kwa TANESCO kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatuliwa haraka ili kurejesha huduma ya umeme kwa wananchi. Amesisitiza kuwa umeme siyo hisani bali ni haki ya wananchi, kwani serikali tayari imefikisha huduma hiyo katika vijiji vyote nchini.

Wananchi wa Ngapapa wameeleza kusikitishwa na hali hiyo, wakisema kuwa kukosekana kwa umeme kumeathiri biashara zao, hasa wale wanaotegemea vifaa vya umeme kama vile mashine za kusaga nafaka, friji za kuhifadhi bidhaa, na vyanzo vya mwangaza wakati wa usiku. Vilevile, wanafunzi wamelazimika kusoma katika mazingira magumu, huku vituo vya afya vikikumbwa na changamoto ya kuhifadhi dawa zinazohitaji ubaridi.

Wananchi hao wameiomba serikali na TANESCO kuchukua hatua za dharura ili kurejesha huduma hiyo muhimu haraka iwezekanavyo.

Post a Comment

0 Comments