F Watu tisa washikiliwa Manyara kwa utapeli mtandaoni. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Watu tisa washikiliwa Manyara kwa utapeli mtandaoni.



Na John Walter -Manyara 

Jeshi la Polisi mkoani Manyara linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kujihusisha na utapeli wa mtandaoni kupitia kampuni inayojulikana kama Lebanet London (LBL).

 Watuhumiwa hao ni watu sita kutoka Wilaya ya Mbulu na watatu kutoka Babati, ambao walikamatwa wakiwa na simu tano, tablets nne na laptop moja zinazodaiwa kutumiwa katika shughuli zao za kihalifu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ahmed Makarani, watuhumiwa hao walikuwa wakitumia mbinu ya kushawishi watu kujiunga na mtandao wa LBL kwa ada inayotofautiana kati ya shilingi 50,000 hadi 540,000 ili kuwa wanachama wa kampuni hiyo.

Upelelezi wa awali umebaini kuwa baada ya mteja kujiunga na mtandao huo, alitumiwa picha mbalimbali za vichekesho, elimu, utafiti, na filamu, ambapo aliahidiwa kupata fedha kila alipofungua maudhui hayo. 

Hata hivyo, uchunguzi umeonyesha kuwa hakuna mtu yeyote kati ya walihojiwa ambaye amewahi kupokea malipo yoyote kama ilivyodaiwa.

Kamanda Makarani amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao mpana wa utapeli huo na kuwachukulia hatua wahusika wote kwa mujibu wa sheria. 

Amewataka wananchi kuwa makini na kuepuka kujiunga na mitandao isiyoeleweka ili kuepuka kutapeliwa.

Jeshi la Polisi limewataka wananchi kutoa taarifa mara moja wanapobaini uwepo wa vitendo vya utapeli wa mtandaoni katika jamii zao ili kusaidia kudhibiti uhalifu huo unaoendelea kushika kasi nchini.

Post a Comment

0 Comments