Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imepokea zawadi ya utambuzi maalum katika Mkutano wa Wakurugenzi wa Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache wa mwaka 2025 kutokana na mchango wake katika kushirikiana na serikali kukuza uchumi wa Tanzania.
Mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo kibaha, uliwaleta pamoja viongozi mbalimbali wa serikali na wadau kutoka sekta binafsi kujadili mikakati ya kuleta maendeleo endelevu. Nafasi ya Airtel Tanzania katika mkutano huu kama mdhamini mkuu, ulidhihirisha azma yake ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini kote.
Akizindua rasmi mkutano huo, Waziri wa nchi ofisi ya raisi - Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alieleza kuwa anatambua mchango wa makampuni ambayo serikali ina hisa chache katika kuunga mkono uchumi wa Tanzania huku akiipongeza Airtel Tanzania kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo ya Tanzania.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuandaa mkutano muhimu na pia napenda kutoa shukrani zangu kwa wadhamini wote, akiwemo Airtel Tanzania kwa mchango wao. Tukio hili linaonyesha mchango umuhimu mkubwa wa ushirikiano wa kimkakati baina ya serikali na sekta binafsi katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi,” alisema Waziri.
Aliongeza “Makampuni ambayo serikali ina hisa chache yameendelea kuwa na mchango mkubwa kwa serikali kupitia magawio ya kila mwaka ambayo yamekuwa kutoka shilingi bilioni 58 kwa mwaka 2019/20 na kufikia shilingi bilioni 195 kwa mwaka 2023/24 na ukuaji mzuri wa zaidi ya asilimia 200. Makampuni haya 17 ambayo serikali ina hisa chache kwa ujumla yanachangia asilimia 33 ya magawio yote kwa serikali kwa mwaka.”
Waziri Mkumbo alisisitiza zaidi kwa Tanzania iko mbioni kukamilisha ajenda ya maendeleo ya mwaka 2050 ambapo sekta binafsi itakuwa na nafasi muhimu ya kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto ambae alikuwa miongoni wa wachangiaji mada kwenye mkutano huo, alitoa shukrani kwa ushiriki wa Airtel Tanzania katika mkutano huo na kueleza namna Airtel Tanzania inavyochagia maendeleo ya kiuchumi.
“Ni heshima kubwa kuwa sehemu ya Mkutano huu. Tunatoa shukrani za dhati kwa Ofisi Msajili wa Hazina kwa kuandaa kusanyiko hili muhimu. Kwa upande wetu Airtel Tanzania, tumelenga kuendelea kutumia teknolojia kikamilifu kuleta maendeleo ya kiuchumi, kuboresha ufanisi wa biashara na kujenga thamani endelevu kwa wadau wetu wote,” alieleza.
Kamoto alidokeza kuwa uwekezaji muhimu uliofanywa na Airtel Tanzania katika miundombinu na teknolojia kwa kutambua kwamba tayari kampuni hiyo imekwisha kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 650 za kitanzania ndani ya miaka mitano iliyopita kwa lengo la kupanua mtandao wetu na kuboresha uzoefu kwa wateja wake.
Aidha, aliongeza zaidi kuwa, “Kwa mwaka 2024 pekee, tuliweka shilingi bilioni 130 katika upanuzi wa miundombinu, na matumizi ya teknolojia ya hali ya juu. Hii inaweka msisitizo kwenye dhamira yetu ya kuboresha uunganishwaji wakati tunahakikisha kuna mapato mazuri kwa ajili ya wawekezaji.”
Nae Mkurugenzi wa Biashara wa Airtel Tanzania, Joseph Muhere, alisisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano endelevu baina ya serikali na sekta binafsikatika maendeleo ya kitaifa.
“Kukutana kwa serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuweka sawa sehemu muhimu za maendeleo kwa Tanzania. Kupitia ushirikiano endelevu, tunaweza kuchochea uvumbuzi, kuboresha fursa za uwekezaji na kujenga masuluhisho endelevu ambayo yanachangia katika ukuaji wa muda mrefu wa taifa, alisema
Mkutano huo wa Wakurugenzi wa Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache wa mwaka 2025 ulimazilika kwa kuweka nia mpya ya sekta binafsi kuchangia katika ushirikiano wa kimkakati baina ya serikali na sekta binafsi. Kupitia wachangiaji wachache kama Airtel Tanzania, Tanzania ipo tayari kupata maendeleo ya kudumu kwa kuhakikisha ujumuishwaji wa kila mwananchi.
0 Comments