Na John Walter -Babati
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amewataka watendaji wa maeneo yanayozungukwa na hifadhi kuwapa wananchi elimu juu ya kulima mazao yasiyowavutia wanyama waharibifu ili kuepuka migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Kaganda ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi magunia 309 ya mahindi kwa vijiji 10 vinavyopakana na hifadhi, mahindi ambayo yamenunuliwa na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU).
Katibu wa JUHIBU, Benson Mwaise, amesema kuwa mahindi hayo yamenunuliwa kwa ajili ya wanachama wa jumuiya hiyo katika vijiji 10 vilivyokubali kuacha kilimo na badala yake kushiriki kwenye uhifadhi.
Mahindi hayo yamegawiwa kwa shule mbalimbali za msingi zilizopo katika kata za Mwada, Nkaiti, na Magara, ili kusaidia chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Mkuu wa wilaya ameagiza wanafunzi waelimishwe kuhusu namna chakula hicho kilivyopatikana, ili wapate uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.
Aidha, Kaganda ameagiza kuandaliwa mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa vijiji vinavyopakana na hifadhi ili kuweka mipaka bayana kati ya shughuli za kilimo na maeneo ya uhifadhi.
Ameeleza kuwa utalii unalipa na wananchi wanapaswa kulima mazao kama tumbaku, ufuta, na aina maalum ya alizeti ambayo hayawavutii wanyama waharibifu.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuweka alama katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utalii ili kuepusha migogoro, pamoja na kuhakikisha mifugo kama ng’ombe haiingii katika maeneo ya hifadhi.
Mkuu wa wilaya amepongeza JUHIBU, wananchi, na viongozi kwa kazi nzuri ya kusimamia uhifadhi na kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali za wanyamapori kwa njia endelevu.
Diwani wa Nkaiti, Steven Saruni Mollel, amepongeza juhudi za JUHIBU akisema kuwa jumuiya hiyo imeleta manufaa makubwa kwa wananchi, ambao sasa wanaelewa thamani ya uhifadhi.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha jamii kunufaika kupitia rasilimali za wanyamapori.
Hatua ya kugawa mahindi hayo inasaidia wazazi na walezi katika kugharamia chakula cha mchana kwa wanafunzi, hasa kutokana na kupungua kwa shughuli za kilimo kwenye vijiji hivyo kutokana na uwekezaji katika uhifadhi.
0 Comments