F Kijiji cha Sangaiwe Chaongoza Kitaifa kwa Ukusanyaji wa Mapato ya Utalii | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kijiji cha Sangaiwe Chaongoza Kitaifa kwa Ukusanyaji wa Mapato ya Utalii


Na John Walter -Babati 

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amepongeza juhudi za Kijiji cha Sangaiwe katika uhifadhi wa mazingira, hatua iliyowafanya kuwa vinara wa kitaifa kwa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na utalii. 

Kaganda amesema kijiji hicho ni mfano wa kuigwa katika Mkoa wa Manyara na Tanzania kwa ujumla kwa mafanikio yake makubwa ya maendeleo.

Kijiji cha Sangaiwe, kilichopo katika Kata ya Mwada, kimepata mafanikio makubwa kutokana na uhifadhi wa wanyamapori. 

Kupitia mapato ya utalii, kijiji kimefanikiwa kuboresha miundombinu na kuinua hali ya maisha ya wakazi wake.

Kwa kutumia mapato hayo Kijiji kimejenga ofisi ya kisasa kwa shughuli za utawala, hatua iliyorahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, Kila kitongoji sasa kina shule ya msingi, huku shule hizo zikiboreshwa kwa madarasa mazuri na walimu wanaolipwa vizuri kwa juhudi za kijiji.

Matokeo mazuri yameonekana kwenye sekta ya elimu, ambapo shule za msingi za kijiji zilishika nafasi ya kwanza na ya nne katika mtihani wa darasa la saba na la nne kwa ngazi ya mkoa mwaka 2024.

Kijiji kinapokea wageni 70-80 kwa siku, huku majirani zao wa Tarangire wakipokea zaidi ya 1,000 kwa siku.

Zahanati ya kisasa imejengwa kwa zaidi ya Shilingi Milioni 200, ikiwa na vifaa tiba na dawa, hatua iliyosifiwa na Mkuu wa Wilaya, Emmanuela Kaganda, kama hatua muhimu kwa afya za wananchi.

Kwa miaka mingi, wakazi wa Sangaiwe walikumbwa na changamoto ya tembo kuharibu mazao yao. 

Hili liliwasukuma kugeuza tatizo hilo kuwa fursa kwa kuingia makubaliano na wawekezaji wa sekta ya malazi ya wageni.

Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU), Patricia Mosea, amesema kijiji kimeanzisha hifadhi za jamii zinazojumuisha vijiji 10 ili kunufaika na uwepo wa tembo badala ya kuwa wahanga wa uharibifu wa mazao.

Wakazi wa Sangaiwe wameonesha uvumilivu wa hali ya juu kwani, licha ya tembo kupita kwenye makazi yao kila siku, wamejifunza kuishi nao bila bughudha huku wakiruhusu wawekezaji kujenga hoteli kwa wageni wanaotembelea kijiji na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Kwa kipindi cha miaka miwili, Shilingi Bilioni 2.4 zimeelekezwa kwenye huduma za jamii kupitia mapato ya utalii.

Hata hivyo, kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu sheria mpya ya mgao wa mapato. 

Awali, vijiji vilikuwa vinapata asilimia 60 ya mapato kutoka kwa wawekezaji, lakini sheria mpya inataka wapewe asilimia 20 pekee.

Diwani wa Kata ya Mwada, Michael Mombo, pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Sangaiwe, Mariani Mwanso, wamesema mabadiliko haya yanawavunja moyo wananchi na wanaomba serikali iendelee na mgao wa asilimia 60 ili maendeleo ya kijiji yaendelee kwa kasi.

Ujenzi wa shule, zahanati, na ofisi ya kijiji ni ushahidi wa jinsi uhifadhi unavyoweza kuinua maisha ya jamii. 

Licha ya changamoto ya tembo na mjadala wa mgao wa mapato, wananchi wa Sangaiwe wanaendelea kufanikisha maendeleo yao kwa kauli mbiu ya Kata ya Mwada "Maendeleo Kwanza, Mambo Mengine Baadaye."  "Tembo kwa Maendeleo."


Post a Comment

0 Comments