Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Lutheran Haydom, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk. Daud Lotto, amesema kambi hiyo ni sehemu ya maadhimisho yatakayofanyika Machi 28 mwaka huu.
"Lengo letu ni kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa afya mara kwa mara," alisema Dk. Lotto.
Zaidi ya wananchi 800 wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu kupitia kambi hiyo, inayotolewa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Manyara na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha.
Katika kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Sikio, Pua na Koo, Dkt. Athanas Budadi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, amewataka wananchi kuacha tabia ya kujisafisha masikio kiholela, kwani inaweza kusababisha madhara makubwa.
"Ni muhimu kufika hospitalini mara moja unapoanza kuhisi maumivu au tatizo lolote la masikio," alisisitiza.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina Mama na Uzazi, Dkt. Colman Mayomba, amewahimiza wazazi kuhakikisha watoto wa kike wanapatiwa chanjo ya HPV ili kujikinga na saratani ya shingo ya kizazi.
"Chanjo hii ni kinga madhubuti dhidi ya ugonjwa huu hatari, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma hii kwa wakati," alisema Dk. Mayomba.
Huduma Zilizotolewa
Kambi hiyo imetoa huduma mbalimbali za kibingwa, zikiwemo:
Magonjwa ya kina mama
Magonjwa ya watoto
Upasuaji mkubwa
Matatizo ya mfumo wa mkojo
Magonjwa ya macho
Magonjwa ya ndani
Matatizo ya mifupa
Magonjwa ya koo, masikio na pua
Uchunguzi wa mionzi
Baadhi ya wananchi waliopata matibabu wameeleza kuridhishwa na huduma hiyo, wakisema imewawezesha kupata matibabu bila kusafiri umbali mrefu.
"Tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha miaka 70, karibu tukuhudumie!"
Aidha, wananchi wameshauriwa kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema na kupata matibabu kwa wakati.
0 Comments