Na John Walter -Babati
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japheth Asunga, ameongoza wajumbe wa kamati hiyo katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji mjini Babati, ambapo wameeleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wake na kuipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) kwa usimamizi mzuri.
Ziara hiyo, iliyofanyika Machi 18, 2025, ilihusisha ukaguzi wa Mradi wa Maji wa Dareda - Singu - Sigino - Bagara pamoja na mradi wa maji taka (Waste Stabilization Pond Layout), ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.6 katika eneo la Maisaka Katani.
Kamati hiyo imepongeza Serikali kwa kutoa shilingi bilioni 17.8 kufanikisha mradi huo mkubwa unaowanufaisha wananchi wa kata za Dareda, Arri, Sigino, Bagara na Maisaka.
Hadi sasa, shilingi bilioni 17.3 tayari zimetumika, huku wajumbe wa kamati wakiiomba Serikali kumalizia kiasi kilichobaki ili kufanikisha upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 mjini Babati.
Kwa sasa, huduma ya maji mjini Babati imefikia asilimia 98, kiwango ambacho kimevuka matarajio ya Ilani ya CCM ya asilimia 95.
Mkurugenzi wa BAWASA, Mhandisi Iddy Yazid Msuya, amesema mamlaka hiyo imefunga mitambo ya kisasa inayosukuma maji muda wote, na itaendelea kusimamia kwa umakini ili wananchi waendelee kupata huduma bora ya maji.
Aidha, Kamati ya PAC na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali wameeleza kuridhishwa na mradi huo, huku wajumbe wa kamati hiyo wakisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuungwa mkono kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.
0 Comments