Na John Walter -Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amewataka wanawake kutokubali vipigo na manyanyaso katika ndoa kwa kisingizio cha uvumilivu.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Hydom, Wilaya ya Mbulu, Sendiga amesisitiza kuwa si kila jambo linapaswa kuvumiliwa katika ndoa.
"Uvumilivu uwe kwa kiasi, ukivumilia vipigo mara ya kwanza, ya pili, ya tatu, atakuua," alisema Sendiga, akiwataka wanawake kuwafundisha watoto wao wa kike kuhusu ndoa kwa kuwaeleza kuwa si kila changamoto inapaswa kustahimiliwa.
Amesema kuwa kivuli cha uvumilivu kimewafanya wanawake wengi kuteseka, huku baadhi yao wakipoteza maisha kwa sababu ya manyanyaso wanayopitia mikononi mwa waume zao au wanaume wanaoishi nao.
Aidha, aliwakumbusha wanaume kuwa hawajaumbwa kuwapiga wanawake, akisisitiza kuwa mwanamke anatoka kwenye ubavu wa mwanaume, hivyo haifai kupigwa.
"Akikupiga ujue huyo si ubavu wako," alisema Sendiga.
Amewataka wazazi kutowalazimisha watoto wa kike waliorejea nyumbani kutokana na manyanyaso kurudi kwenye ndoa hizo kwa sababu tu ya kuwa na watoto.
"Kuwa na watoto isiwe sababu ya kuvumilia mateso," aliongeza Sendiga.
Pia, amewahimiza wanawake kutumia majukwaa yao kuwaambia wenzao ukweli kuhusu madhara ya manyanyaso ya kijinsia, ili kusaidia kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Mwanamke Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji."
0 Comments