F Ripoti Ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii Katika Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto Yaonesha Changamoto Kadhaa Babati | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ripoti Ya Ufuatiliaji wa Uwajibikaji wa Jamii Katika Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto Yaonesha Changamoto Kadhaa Babati

Na John Walter -Babati 

Marafiki wa Elimu wilaya ya Babati wamewasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa jamii katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto.

Ripoti hiyo, iliyowasilishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Benjamin Richard, inaonesha changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto katika malezi, usalama, na mazingira ya kujifunzia.

Utafiti huu ulifanyika katika kata nne za Babati ,Bagara, Maisaka na Nangara kwenye shule za Msingi 16, ambapo wadau mbalimbali walihojiwa, wakiwemo watendaji wa kata, wamiliki wa vituo vya kulelea watoto (day care), walimu, wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa serikali za mitaa na vijiji, pamoja na wazazi wenye watoto katika shule za awali.

Matokeo Muhimu ya Ripoti

  1. Usalama wa Watoto Shuleni

    • Kati ya shule 16 zilizotembelewa, hakuna hata moja yenye uzio, hali inayohatarisha usalama wa watoto.
    • Shule nyingi zipo karibu na barabara, hivyo kuongeza hatari kwa watoto.
  2. Adhabu kwa Watoto

    • Asilimia 11.2 ya waliohojiwa walithibitisha kuwepo kwa adhabu za kuumiza katika baadhi ya shule.
    • Hata hivyo, asilimia 60 ya wazazi na walimu walikiri kuwa shule ni salama na wanatambua umuhimu wa ulinzi na usalama wa watoto.
  3. Afya na Mazingira ya Shule

    • Asilimia 68 ya vyoo vya shule si salama kwa watoto, hali inayohatarisha afya zao.
    • Ni shule tano pekee ndizo zenye vyoo maalum kwa wanafunzi wa awali.
  4. Malezi na Muda wa Wazazi na Watoto

    • Asilimia 93.7 ya watu 168 waliohojiwa walikiri kuwa wazazi wengi hawana muda wa kukaa au kucheza na watoto wao.
    • Wazazi wengi wamekuwa wakiacha majukumu yao kwa wafanyakazi wa ndani, ambao mara nyingi huonekana kama mama na baba wa watoto hao.

Hatua Zinazochukuliwa

Baada ya uwasilishaji wa ripoti hii, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Marafiki wa Elimu Babati, Gaudencia Igoshalimo, amesema kuwa watarejea kwa wananchi kwa ajili ya kuhamasisha marekebisho ya changamoto zilizobainika.

Marafiki wa Elimu Babati, chini ya mwavuli wa HakiElimu, wanatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha mazingira ya watoto, ikiwa ni pamoja na:

  • Ujenzi wa vyoo katika shule tano ili kuboresha usafi na usalama wa wanafunzi.
  • Ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Nakwa, ambapo wazazi watachangia ujenzi wa msingi na HakiElimu itakamilisha mradi huo.

Wito kwa Wazazi

Wazazi wametakiwa kutenga muda wa kukaa na watoto wao badala ya kuwaachia malezi kwa wafanyakazi wa ndani pekee.

 “Wazazi waache tabia ya kuwa bize na maisha huku wakitelekeza watoto wao, ni jukumu la mzazi kuhakikisha mtoto anapata malezi bora na muda wa kufundwa katika misingi sahihi ya maisha,” ilisisitizwa katika ripoti hiyo.

Kwa hatua hii, Marafiki wa Elimu Babati wanaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira salama, yenye afya, na yanayochochea maendeleo yao ya elimu na maisha kwa ujumla.

Picha mbalimbali wakati wa Uwasilishaji ripoti.








Post a Comment

0 Comments