Na John Walter -Manyara
Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Manyara imefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani kwa kujenga vituo vya kuchotea maji vya umma 3,804 pamoja na kufanya maunganisho ya maji majumbani kwa kaya 6,172 katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Mwanamke Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Haydom, wilayani Mbulu, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema kuwa jitihada hizi ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya maji na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinazolenga kumrahisishia mwanamke huduma za maji safi na salama karibu na makazi yake.
“Mwanamke ndiye anayebeba mzigo mkubwa wa kuchota maji, hivyo serikali imehakikisha kuwa anatembea umbali mfupi kupata huduma hii muhimu.
Hili limeokoa muda, kupunguza gharama na hata kusaidia kuimarisha ndoa, kwani sasa wanawake wanatumia muda mwingi zaidi kwenye shughuli za maendeleo badala ya kutafuta maji,” alisema Queen Sendiga.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa RUWASA Mkoa wa Manyara, Amina Mwanja, alieleza kuwa uboreshaji wa huduma za maji vijijini umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wanawake.
“Wanawake sasa wanatumia muda wao kwa shughuli nyingine za kiuchumi na za kifamilia, jambo ambalo limeongeza ustawi wa jamii kwa ujumla,” alisema.
RUWASA inaendelea na jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kila mwananchi, hasa wa vijijini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuboresha maisha ya Watanzania.
0 Comments