Na John Walter -Hanang'
Serikali imeendelea kuimarisha huduma muhimu za kijamii kwa kurejesha miradi ya maji katika Wilaya ya Hanang’, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 19 zilitengwa kwa miradi hiyo mwaka 2024 mkoani Manyara.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, akishushuhudia utiaji Saini miradi mitatu kati ya wakandarasi na RUWASA mkoa wa Manyara, machi 30,2025, amewataka wakandarasi walioshinda zabuni za miradi hiyo kuhakikisha wanatekeleza kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa katika mikataba yao.
Ameeleza kuwa hakuna nafasi ya kuongezewa muda wa utekelezaji wa miradi hiyo (extension), na kwamba ni lazima mikataba ifanyiwe kazi kama ilivyopangwa ili wananchi waendelee kupata huduma za maji safi na salama bila usumbufu.
“Mkoa wa Manyara ni marufuku kuongezwa muda wa miradi, mikataba iliyosainiwa lazima ifanyiwe kazi, miradi isisimame kwa namna yoyote ili wananchi wapate huduma, kina mama wapumzike kubeba ndoo kichwani,” alisema Sendiga.
Ameongeza kuwa wakandarasi hao wanapaswa kutoa ajira kwa wananchi wa eneo husika, ili kusaidia kukuza uchumi wa maeneo hayo na kuwafanya wananchi washiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, Mhandisi James Kionaumela, mikataba mitatu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.6 imesainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika kata za Gendabi na Dawar ambapo Kampuni zilizopewa zabuni hizo ni:
M/S URSINO LTD – Ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka chanzo cha Mto Dumanang’ kwa ushirikiano na RUWASA.
OCTAL Group Ltd – Usambazaji wa mabomba ya plastiki (HDPE Pipes).
SOLOHOGA Company LTD – Usambazaji wa mabomba ya chuma (GS Pipes).
Mhandisi Kionaumela amesema miradi hiyo ikikamilika, kiwango cha upatikanaji wa maji wilayani Hanang’ kitaongezeka hadi kufikia asilimia 95.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa URSINO Ltd, Mhandisi Mnandi M. Mnandi, ameishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa nafasi kwa wakandarasi wa ndani kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wilaya ya Hanang’ ilikumbwa na maafa mwaka 2023 kutokana na maporomoko ya maji, mawe, tope, na miti, na kuharibu miundombinu yote ya maji, hivyo miradi hii inatajwa kuwa mwarobaini wa changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.
0 Comments