Na John Walter -Babati
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Manyara ili kuwawezesha kuelewa na kuandika kwa usahihi masuala ya haki za binadamu.
Mafunzo hayo yamefanyika Leo katika ukumbi kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara leo Machi 19,2025 katika jitihada za kuhakikisha wananchi wanatambua haki zao na kuhimiza uwajibikaji katika jamii.
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohammed Hamadi, amesema kuwa mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa tume kufikisha elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Amesisitiza kuwa watu wakitambua haki zao, wataheshimu haki za binadamu na kusaidia kujenga jamii yenye usawa na haki.
Pamoja na mafunzo kwa waandishi wa habari, tume pia itatembelea shule mbalimbali ili kutoa elimu juu ya haki za watoto.
Hatua hii inalenga kuwajengea watoto uelewa wa haki zao na kuwasaidia kujilinda dhidi ya ukiukwaji wa haki hizo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Khalifan Botea, Afisa Uchunguzi wa tume, amesema kuwa bado kuna mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zinachangia uvunjifu wa haki za binadamu.


Ameeleza kuwa jamii ina wajibu wa kuhakikisha haki za binadamu, hususan kwa makundi maalum kama walemavu, watoto na wazee, zinalindwa.
Tume hiyo pia inapanga kutembelea vituo vya polisi na magereza ili kuhakikisha haki za watuhumiwa na wafungwa zinalindwa.
Aidha, watakutana na watendaji wa mitaa na vijiji, kwa kuwa wao ndio wenye nafasi kubwa ya kuwafikia wananchi moja kwa moja.
Katika ziara yao, tume pia itafanya mikutano ya hadhara ili kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu haki zao.
Wananchi wameshukuru serikali kwa kuiwezesha tume kufika maeneo mbalimbali nchini na kutoa elimu hii muhimu.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni chombo cha serikali chenye jukumu la kulinda na kusimamia haki za binadamu nchini Tanzania.
0 Comments