F Ujenzi wa Majengo Mapya Hospitali ya Mji wa Babati Wafikia Asilimia 98 | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ujenzi wa Majengo Mapya Hospitali ya Mji wa Babati Wafikia Asilimia 98


Na John Walter -Babati.

Ujenzi wa majengo mapya katika Hospitali ya Mji wa Babati umefikia asilimia 98 kutokana na ufuatiliaji wa karibu wa Halmashauri ya Mji wa Babati.

Haya yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Shabani Mpendu, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi huo kwa Kamati ya ALAT mkoa wa Manyara.

Majengo hayo mapya yanajumuisha jengo la mionzi, maabara, jengo la kufulia nguo, jengo la wagonjwa wa nje, na kichomea taka. 

Kwa mujibu wa Mpendu, hatua inayofuata ni ujenzi wa njia za wapita kwa miguu na ukuta kwa upande wa nyuma uliosalia, pamoja na ujenzi wa wodi mbili za wanaume na wanawake ili kuboresha zaidi huduma kwa wananchi.

Katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Machi 7, 2025, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) mkoa wa Manyara, Peter Sulle, amepongeza serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi. 

Alisema kuwa serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi yake ya kuboresha huduma za afya Manyara.

Kamati ya ALAT mkoa wa Manyara imeipongeza Halmashauri ya Mji wa Babati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, ambapo thamani ya fedha imeonekana. 

Serikali ilitoa shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo matano, hatua inayolenga kuimarisha huduma katika hospitali hiyo kongwe inayohudumia wakazi wa Babati na maeneo jirani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shabani Mpendu, ameeleza kuwa huduma kwa wateja zimeboreshwa, ambapo baadhi ya watumishi wazembe walifukuzwa au kuhamishwa. 

Aidha, ameagiza Mganga Mkuu wa hospitali hiyo aanzishe mafunzo ya huduma kwa wateja kwa watumishi wote ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Afisa Tarafa wa Babati, Hassan Msalla, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, ameihakikishia kamati ya ALAT kuwa miradi yote ya serikali inasimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Mheshimiwa Paulina Gekul, amesema kuwa maendeleo hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya madiwani na serikali, jambo linalowezesha miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Nasibu Msuya, amesema kuwa wataendelea kusimamia utoaji wa huduma bora hospitalini hapo na kuondoa changamoto za malalamiko kwa wateja.

Amebainisha kuwa wameanzisha kundi sogozi litakalowapa wananchi fursa ya kutoa maoni na malalamiko yao ili kuboresha huduma hospitalini hapo.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa ALAT mkoa wa Manyara wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha kuboreshwa kwa huduma za afya katika hospitali ya mji wa Babati.

Post a Comment

0 Comments