Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe wamelaani vikali tukio la kupigwa kwa katibu Mwenezi wa Baraza la wanawake Chadema Taifa (BAWACHA) Sigrada Mligo kilichofanywa Machi 25 Mwaka huu na anayedaiwa kuwa ni mlinzi wa Chama hicho wakati wa vikao vya ndani.
UWT kupitia mwenyekiti Dkt.Scholastika Kevela amelaani kitendo hicho walipofika katika kijiji cha Kisilo kata ya Lugenge halmashauri ya mji wa Njombe nyumbani kwa Sigrada baada ya maelekezo ya Katibu Mwenezi wao Amos Makala pamoja na Mwenyekiti wa UWT Mary Chatanda na kwamba jambo hilo linapaswa kupigwa vita na kila mtanzania.
"Haya ya kuchapana ngumi hatujazoea,tunalaani kitendo hiki cha kupigwa kiongozi mkubwa na mwenye heshima ya kitaifa na mtu akitoa hoja yapaswa asikilizwe"amesema Scholastika
Ametoa wito kwa Mwenezi BAWACHA kutokata tamaa na kurudishwa nyuma badala yake aweze kuongeza nguvu ili kwenda kuwapigania wanawake wa Tanzania na kuliomba jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhimiwa anakamatwa kwa ajili ya hatua za kisheria
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Deo Sanga amesema atahakikisha vitendo hivyo haviwezi kujirudia katika mkoa wa Njombe huku kwa sasa wanaendelea kuwa bega kwa bega na Mwenezi BAWACHA ili kuimarisha afya yake ambapo kwa sasa amekwisha toka katika hospitali ya mji wa Njombe na anatarajia kwenda katika hospital nyingine kwa uchunguzi zaidi.
Awali katibu wa CCM mkoa wa Njombe Julius Peter amesema baada ya maelekezo ya CCM taifa wamefika Nyumbani kwa Sigrada na kumjulia hali huku wakiwataka watanzania kuendelea kudumisha amani badala ya kuendekeza ugomvi na vurugu.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Baraza la wanawake Chadema Taifa Sigrada Mligo anasema kwa sasa anaendelea vizuri ambapo anatarajia kwenda katika katika hospital kubwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku akishukuru uongozi wa UWT kwa kufika nyumbani na kumjulia hali.
0 Comments