Na John Walter -Babati
Katika tukio la kusikitisha na la kinyama lililotokea kijijini Orongadida, kata ya Qash, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, kijana aitwaye Jamal Yusuph (28) anadaiwa kumuua mama yake mzazi, Zauda Shabani (57), kwa kumchinja shingoni kwa kutumia kisu, kufuatia mgogoro wa kifamilia uliodumu kwa muda mrefu.
Tukio hilo limetokea Aprili 12, 2025, majira ya saa 4:00 asubuhi, ambapo inadaiwa kuwa kijana huyo ambaye ni mtumiaji wa dawa za kulevya aina ya bangi, alikuwa akigombana mara kwa mara na mama yake kuhusu umiliki wa nyumba wanayoishi.
Jamal alitaka mama yake aondoke ili yeye abaki kuimiliki nyumba hiyo.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo ya kikatili, nje ya nyumba Jamal alikutana na mmoja wa ndugu zake na kumwambia: "Njoo umuone dada yako, nimeshamuua." Hata hivyo, hakujua kuwa kitendo hicho kingemgeukia muda mfupi baadaye.
Wananchi waliopata taarifa za tukio hilo waliwahi kufika eneo la tukio wakiwa na hasira kali, wakavunja mlango wa nyumba aliyojificha mtuhumiwa na kuanza kumshambulia kwa mawe.
Licha ya jitihada za baadhi ya viongozi wa mtaa kumzuia, wananchi hao walifanikiwa kumtoa nje na kumshambulia na baadaye kupoteza maisha.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kinyasi, Andrea Peter Darabe, ameeleza kuwa alimkamata kijana huyo na kumuweka chini ya ulinzi lakini ghadhabu ya wananchi ilizidi nguvu.
Aidha, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mji Mpya, Bakari Hamisi, amesema kuwa mgogoro kati ya Jamal na mama yake ulikuwa wa muda mrefu na juhudi za upatanisho zilifanyika mara kadhaa bila mafanikio.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bi. Emmanuela Kaganda, amelaani vikali tukio hilo akisema: "Ukatili huu ni wa kusikitisha na ni changamoto kubwa kwa jamii, hata hivyo, wananchi wanapaswa kufuata sheria na siyo kujichukulia sheria mkononi."


Miili ya marehemu wote wawili imehifadhiwa katika hospitali ya mji wa wa Babati Mrara kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo.
Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa Orongadida na kuzua maswali mengi kuhusu mmomonyoko wa maadili kwa vijana na nafasi ya familia katika malezi.
0 Comments