Na John Walter -Babati
Katika kuadhimisha Siku ya Madaktari wa Wanyama Duniani, katibu msaidizi wa chama cha madaktari wa mifugo Tanzania kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dr.Caroline Uronu, ameongoza wanachama wa chama hicho kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kliniki binafsi za mifugo, makampuni makubwa ya dawa za mifugo na mashirika mbalimbali katika kutoa huduma kwa jamii kama sehemu ya shukrani kwa taaluma waliyoipata.
Maadhimisho haya yanayofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi Aprili tangu kuanzishwa rasmi na Jumuiya ya Madaktari wa Wanyama Duniani mwaka 2000, mwaka huu yanafanyika katika Kanda ya Kaskazini na Kati.
Mikoa inayoshiriki ni pamoja na Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Manyara na Arusha.
Katika Mkoa wa Manyara, madaktari wa mifugo wamekuwa wakitoa huduma ya afya kwa mifugo kwa muda wa siku tatu mfululizo, huduma ambazo ni bure kabisa kwa wananchi.
Huduma hizo zinahusisha matibabu, chanjo, upasuaji mkubwa kwa mbwa na paka, pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu taaluma ya udaktari wa wanyama.
Huduma hizo zimekuwa zikitolewa katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati, huku timu nyingine za wataalamu wakitembelea mitaa na vijiji mbalimbali, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mbulu Mji, Hanang’, Babati Mji na Babati Wilaya, kuhakikisha jamii pana inafikiwa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Afya ya Mnyama ni Jukumu la Pamoja”, ikisisitiza ushirikiano kati ya jamii na wataalamu katika kuhakikisha ustawi wa wanyama ambao ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu na uchumi wa taifa.
Sherehe za kilele cha maadhimisho hayo zinatarajiwa kufanyika kesho, Aprili 26, ambapo wananchi wengi wanatarajiwa kuhudhuria kupata huduma na elimu zaidi kuhusu afya ya mifugo yao.
Kwa mujibu wa Dr.Caroline Uronu, dhamira ya maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii kuelewa umuhimu wa afya ya wanyama na mchango wa madaktari wa mifugo katika maendeleo ya sekta ya mifugo na afya ya jamii kwa ujumla.
0 Comments