F Pentagon FC yakubali mziki wa Utalingolo FC | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Pentagon FC yakubali mziki wa Utalingolo FC

 


Timu ya Pentagon FC ya Jijini Mbeya inayoshiriki ligi daraja la tatu  imekubali kichapo cha goli moja kwa sifuri dhidi ya timu ya kata ya Utalingolo FC ya mkoani Njombe katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa Iyunga Sekondari jijini humo.

Wakizungumza mara baada ya kuibuka na ushindi huo baadhi ya viongozi wa kata ya Utalingolo akiwemo Elia Chilatu afisa Mtendaji wa kijiji cha Utalingolo pamoja na Renatus Mgani ambaye ni Afisa Mtendaji wa kata hiyo wanasema ushindi huo umekuwa ni chachu kubwa kwao kuelekea kwenye mashindano mengine mkoani Njombe.

"Kuja huku ni moja ya maandalizi ya  mashindano ya Mwanyika Cup yanayoenda kuanza tarehe tisa ambapo sisi ni mabingwa watetezi na tumedhamiria kwenda kutetea ubingwa wetu ndio maana tumekuja huku ili kufanya maandalizi ya kutosha"amesema Chilatu

Delbet Ngole ni Kamptain wa Utalingolo FC Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo amesema maandalizi yao kwa sasa yamekamilika kuingia kwenye mashindano.

"Tumemaliza mchezo wetu hapa salama lakini tunamshukuru Diwani wetu Erasto Mpete kwa kutuwezesha ziara yetu kwa ajili ya maandalizi ya ligi ya Mbunge, kwa kuwa hapa tumekutana na kipimo kizuri"amesema Ngole

Yohana Homba ni mwalimu wa Pentagon FC amefurahishwa na mchezo huo uliozidi kuimarisha ushirikiano baina ya timu hizo zinazotoka mikoa tofauti.

"Jambo lililofanyika hapa ni zuri na sisi tumetamani kufika halmashauri ya mji wa Njombe kwasababu ya hii changamoto waliotuonyesha"amesema Homba

Baadhi ya mashabiki waliosafiri na timu wamefurahishwa na kiwango cha timu yao huku wakimpongeza diwani kwa kuwaandalia ziara hiyo ambayo imekuwa kubwa kwao.

Kufika kwa Timu hiyo jijini Mbeya ni ahadi ya diwani wa kata ya Utalingolo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Njombe Erasto Mpete,kutoka nje ya mkoa na kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Uwanja wa Sokoine unaotumika kwenye michezo ya ligi kuu na hii ni baada ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye mashindano ya msimu wa mwaka wa 2024 ya ligi ya Mbunge wa Njombe mjini Mwanyika CUP ambapo timu hiyo iliibuka mabingwa. 

Post a Comment

0 Comments