F Serikali yapongezwa kwa mageuzi makubwa sekta ya afya Mbulu mji | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yapongezwa kwa mageuzi makubwa sekta ya afya Mbulu mji



Na John Walter -Mbulu 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Bi. Rehema Said Bwasi, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, hususan katika sekta ya afya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bi. Bwasi amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Halmashauri ya Mji wa Mbulu imepokea kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya maboresho ya huduma za afya. 

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 500 zilitumika kujenga Kituo cha Afya cha Kainam ambacho kwa sasa kimeanza kutoa huduma kwa wananchi.

Aidha, amesema kiasi cha shilingi milioni 900 kimetumika kukarabati Hospitali ya Mji wa Mbulu ambayo ni ya muda mrefu, ambapo maboresho yaliyofanyika ni pamoja na ujenzi wa jengo la mama na mtoto, jengo la kufulia, uzio, kichomea taka, njia za waenda kwa miguu, jengo la dharura, jengo la wagonjwa mahututi pamoja na ununuzi wa vifaa vyake. 

Pia, miundombinu chakavu ya maji safi na maji taka imebadilishwa ili kuhakikisha mazingira bora ya utoaji huduma.

“Kwa sasa Hospitali ya Mji wa Mbulu ina muonekano mzuri sana, na kutokana na maboresho haya makubwa, idadi ya rufaa imepungua kwa kiwango kikubwa, hivyo kuwapunguzia wananchi gharama za matibabu,” alisema Bi. Bwasi.

Wananchi waliohojiwa wamesema kuwa huduma ya mama na mtoto imeimarika sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, na sasa hawalazimiki tena kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo huku wakimshukuru Rais Samia kwa kugusa maisha yao moja kwa moja.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Dkt. Martine Loay, amesema kuwa kwa sasa hospitali hiyo inalaza wagonjwa kati ya 80 hadi 100 kwa siku na inahudumia wananchi wengi kutokana na uboreshwaji wa huduma.

Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo ina hospitali moja, vituo vya afya viwili, na zahanati 19 za serikali,  watumishi wa idara ya afya ni 291, wakiwemo 30 waliopatikana kupitia ajira mpya.

Dkt. Loay pia ameeleza kuwa wamepokea gari jipya la kubebea wagonjwa ambalo limepelekwa katika Kituo cha Afya cha Daudi, hatua ambayo imeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za dharura.

Wananchi wa Mbulu wameendelea kuishukuru serikali kwa jitihada zake za kuimarisha sekta ya afya na kuonyesha kwa vitendo kuwa inajali afya za wananchi wake.

Post a Comment

0 Comments