Katika kuendelea kukuza elimu na kutoa motisha kwa wanafunzi, shule ya Deira English Medium iliyopo mjini Babati mkoani Manyara imeandaa hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wake waliowahi kusoma katika shule hiyo na kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne mwaka 2024.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Mhandisi Nada Shauri, ametoa hundi ya shilingi laki tano kwa wanafunzi tisa waliopata daraja la kwanza (Division One) na alama za single digits katika shule zao za sekondari walizohitimu nazo.
Wanafunzi hao walihitimu darasa la saba katika shule ya Deira mwaka 2020.
Katika hotuba yake, Mhandisi Nada aliahidi kuwa motisha na zawadi kwa wanafunzi bora itaendelea kutolewa si tu wakiwa ndani ya shule, bali hata baada ya kuhitimu, kama njia ya kuendeleza ushawishi chanya na ufuatiliaji wa mafanikio yao.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara - Idara ya Elimu, Shabani Gwandu, alipongeza ubunifu huo wa kuweka ahadi kwa wanafunzi kama njia ya kuwahamasisha kufanya vizuri.
Alisema shule hiyo imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na matokeo bora na nidhamu ya hali ya juu.
Shule hiyo, ambayo haijawahi kushuka nje ya tatu bora kimkoa katika Halmashauri zote saba za mkoa wa Manyara, inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kutangaza mkoa kupitia matokeo bora na malezi bora kwa wanafunzi wake.
Mwaka 2024, shule hiyo ilitoa wanafunzi wengi waliopata daraja la kwanza, ikiwa ni ushahidi wa ubora wake.
Mbali na wanafunzi waliomaliza, pia wanafunzi waliopo walipata zawadi mbalimbali; wakiwemo wa darasa la tano waliokabidhiwa bahasha ya shilingi elfu hamsini (50,000), kalamu na madaftari kama motisha ya kuongeza bidii zaidi baada ya kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa ya darasa la nne mwaka Jana.
Meneja wa shule hiyo, Mwalimu Gasper Apolnary, alieleza kuwa siri ya mafanikio hayo ni nidhamu, walimu kujituma na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Alisema shule hiyo imejenga misingi imara ya kitaaluma na kimaadili tangu awali, jambo linaloendelea kuzaa matunda.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Simon Mumbee, aliipongeza shule hiyo kwa kuutangaza vyema mkoa wa Manyara na mji wa Babati kupitia matokeo bora na ushindani wa kweli.
Katika hatua nyingine, wanafunzi wote waliopata zawadi watafunguliwa akaunti bure na benki ya NMB, tawi la Babati, kama sehemu ya kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba na usimamizi wa fedha.
Kwa sasa, wanafunzi wa shule hiyo wapo kwenye likizo fupi ya Pasaka na wanatarajiwa kurejea kuendelea na masomo baada ya sikukuu.
Wazazi, walezi na wadau wa elimu wanakaribishwa kuwasiliana na uongozi wa shule kwa namba 0717360037 au 0752878704 kwa taarifa zaidi.
0 Comments