Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Philipo Mwakibete, ametoa wito kwa Wafanyabiashara wote ndani ya Manispaa hiyo kuhakikisha wanalipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, hasa kipindi hiki cha kuelekea mabadiliko ya bajeti ya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2025 katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Bw. Mwakibete alisisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni wajibu wa kila mfanyabiashara na ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
"Kwa kuwa imesalia takribani miezi miwili kabla ya bajeti mpya ya Serikali kuanza kutekelezwa, tunawakumbusha wafanyabiashara wote kuhakikisha wanalipa kodi zao mapema ili kuepuka adhabu au faini zitokanazo na ucheleweshaji. Hili si tu suala la kuepuka usumbufu, bali ni sehemu ya uzalendo na mchango katika maendeleo ya nchi yetu. "
Aidha, alitoa rai kwa Wafanyabiashara wanaomiliki baa pamoja na wauzaji wa vinywaji kuhakikisha wanakata leseni halali za biashara kama inavyotakiwa kisheria. Alibainisha kuwa kufuata taratibu za kisheria si tu kunarahisisha usimamizi wa biashara, bali pia kunalinda ustawi wa jamii kwa ujumla.
"Wafanyabiashara wanapaswa kuelewa kuwa kupata leseni ni hatua ya msingi ya kuendesha biashara kwa mujibu wa sheria. Hii huwasaidia kuepuka migogoro na mamlaka za usimamizi, na pia hutoa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya Manispaa yetu," aliongeza.
0 Comments