F Wananchi wa Kiru Dick wapongeza jitihada za DC Babati kutatua migogoro. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Wananchi wa Kiru Dick wapongeza jitihada za DC Babati kutatua migogoro.


Na John Walter -Babati 
Wananchi wa Kiru Diki, Wilaya ya Babati, wameonyesha furaha na shukrani zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, kwa juhudi zake zilizofanikisha kurejeshwa kwa amani katika eneo lao baada ya miaka kadhaa ya migogoro na mvutano kati yao na wawekezaji.

Hali hiyo ilidhihirika wazi Aprili 26, 2025, katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kiru Diki, uliofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wananchi hao walibubujikwa na maneno ya furaha, wakikiri hadharani kuwa sasa wanaishi kwa amani na utulivu mkubwa.

Kwa miaka mingi, Kiru Diki imekuwa ikikumbwa na migogoro ya ardhi iliyosababisha sintofahamu na ukosefu wa amani. Hata hivyo, baada ya Mkuu wa Wilaya kuingilia kati, kusimama kidete kutafuta haki, na kufanya ziara za mara kwa mara kwa ajili ya kutoa elimu na kujenga uelewa kwa wananchi, hali imebadilika na eneo hilo sasa linashuhudia utulivu wa kipekee.

Katika mkutano huo, Mhe. Kaganda alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maendeleo kwa ajili ya kujenga Kiru mpya iliyo imara na yenye matumaini mapya. Aidha, kama sehemu ya kuhamasisha mshikamano kwa vijana, alikabidhi mipira mitano na seti ya jezi kwa ajili ya kuimarisha timu zao za michezo, akibainisha kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kukuza amani na mshikamano katika jamii.

Miongoni mwa wananchi waliomshukuru na kumpongeza DC Kaganda ni Mama Rashid, mkazi wa eneo hilo, ambaye alieleza kuwa: *"Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, tunajisikia salama na tunashukuru sana kwa juhudi hizi."* Pia walikuwepo Mzee Severini Awadhi, Hamisi Almasi na Bi. Anna Ibrahimu, ambao kwa nyakati tofauti walimpongeza Mhe. Kaganda kwa uongozi wake wa karibu na wananchi, na msimamo wake wa kulinda maslahi ya wananchi wa Kiru Diki.

Kwa sasa, wananchi wa Kiru Diki wanaendelea kujenga maisha yao kwa matumaini mapya, wakiamini kuwa kwa mshikamano na uongozi bora, maendeleo zaidi yanakuja.

Post a Comment

0 Comments