F Ziara ya RC Manyara wilayani Hanang' yawaletea Wananchi matumaini. | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ziara ya RC Manyara wilayani Hanang' yawaletea Wananchi matumaini.


Na John Walter -Manyara

Ziara ya siku nne ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, wilayani Hanang’ imeleta matumaini makubwa kwa wananchi, hasa katika sekta ya afya, miundombinu ya barabara, maji, na umeme.

Katika kijiji cha Muungano, kata ya Laghanga, Mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa zahanati ya kijiji hicho ianze kuhudumia wananchi ifikapo Aprili 30 mwaka huu, akiahidi kurejea mwenyewe kwa ajili ya kuizindua rasmi.

Katika ziara hiyo, Sendiga aliambatana na wataalamu kutoka TANESCO, RUWASA, na BAWASA, ambao waliwahakikishia wananchi kuwa changamoto za maji, umeme, na barabara zitatatuliwa kwa haraka kama alivyoelekeza.

Mkuu wa Mkoa alitembelea kata mbalimbali zenye changamoto za miundombinu, zikiwemo Dumbeta, Laghanga, Ishponga, Gehandu, Gitting, Nangwa, Mogitu, Katesh, Jorodom, Ganana, Endasak, na Dirma.

Katika maeneo yote aliyopita, Sendiga aliwasikiliza wananchi moja kwa moja ili kufahamu matatizo yao na kuwapa majibu papo hapo. 

Wananchi walimpokea kwa shangwe na nderemo, wakicheza ngoma zao za asili, huku wengine wakisimama barabarani kumsalimia.

Akizungumzia umuhimu wa ziara yake, Sendiga alisema kuwa yeye ni msaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ni wajibu wake kufuatilia miradi inayotekelezwa na kujiridhisha kuwa fedha za serikali zinatumika kwa manufaa ya wananchi.

Ziara hiyo pia imechochea kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Hanang', ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa nyumba za walimu, ujenzi wa ofisi za walimu, madarasa, maabara, zahanati, na vyoo vya wanafunzi

Sendiga aliwahimiza wataalamu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Wananchi wamesifu mtindo wa uongozi wa Mkuu wa Mkoa, wakisema wanapenda viongozi wanaowatembelea na kuwasikiliza moja kwa moja, badala ya wanaokaa maofisini bila kushuka kwa wananchi.

Kwa kaulimbiu yake ya “Sifungui buti mpaka kieleweke – Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”, Sendiga amesisitiza kuwa ataendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote wa Manyara.

Aidha Sendiga, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ni jukumu la viongozi wa mikoa na wilaya kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa kwa ufanisi ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments